HAPI AITAKA MMG KUTEKELEZA MAAGIZO YA SERIKALI
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameutaka Mgodi wa Dhahabu wa MMG Limited kutekeleza maagizo ya serikali yanayotolewa kwa mujibu wa sheria mbalimbali zinazosimamia sekta ya madini hapa nchini.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 19 Julai, 2022 wakati alipoutembelea mgodi huo uliopo katika Kijiji cha Seka, katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kuutaka kutoa maelezo ya kukiuka maagizo yake aliyotoa awali.
“Ninataka mgodi utoe maelezo kwa nini haujatekeleza maagizo yangu na maagizo ya ofisi ya madini Mkoa wa Mara kuhusu kulipa ushuru wa huduma, kuwa na mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) na kuwa na Meneja Mkuu wa Kampuni” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa ushuru wa huduma na CSR sio msaada, ni masuala ya kisheria lazima yatekelezwe na wawekezaji wote hapa nchini kwa ajili ya maendeleo ya Halmashauri hiyo.
Wakati huo huo, Mheshimiwa hapi ameuagiza mgodi huo kuandaa mpango wa kufunga mgodi huo kwa mujibu wa sheria na kuutaka mgodi huo kuwasilisha majina ya kampuni, thamani ya zabuni walizopewa na muda wa utekelezaji ili wazabuni hao waweze kulipa ushuru wa huduma na CSR kwa Halmashauri.
Mheshimiwa Hapi pia ameushauri mgodi huo kujenga uzio kuzunguka eneo lake ili kuzuia uhalifu unaoweza kujitokeza kwa kuwa hauna uzio katika sehemu kubwa ya mgodi huo.
Mheshimiwa Hapi ameutaka mgodi huo kumlipa Bibi Sharma Mwanyoka mjasiriamali ambaye alikuwa anafanya biashara na mgodi huo ambaye anadai shilingi milioni 5 kuanzia mwaka 2018.
Aidha, ameutaka mgodi huo kuajiri Afisa Uhusiano ili kuweka mahusiano mazuri na wananchi wanauzunguka mgodi huo na kuachana na mfumo wa sasa ambapo Meneja wa Utawala ndiye Mhasibu, mtu wa utawala na Afisa Uhusiano mtu mmoja.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkoa wa Mara Mhandisi Joseph Kumburu ameeleza kuwa katika ukaguzi wa wataalamu wa madini katika mgodi huo, waliagiza mgodi huo kumteua Meneja Mkuu ambaye kwa mujibu wa Sheria za Madini ndiye mtu wa kuzungumza na serikali.
“Kwa sasa, hawana mtu mwenye cheo hicho na kila wakiitwa kwa jambo fulani wanamleta afisa tofauti kwenda kusilikiliza na tuliwapa muda wa siku 30 zimeshaisha lakini suala hilo halijatekelezwa” alisema Mhandisi Kumburu.
Aidha, Mhandisi Kumburu ameeleza kuwa mgodi ulikuwa umeelekezwa kununua mavazi zaidi ya usalama (PPE) kwa ajili ya wafanyakazi lakini hawajatekeleza.
Bwana Kumburu ameeleza kuwa mgodi huo uliagiza pia kumwaga maji katika barabara zake ili kupunguza vumbi kwa wananchi wanaouzunguka mgodi huo ambalo halijatekelezwa.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa, kamati ya usalama ya Mkoa, Wilaya ya Musoma na baadhi ya watumishi kutoka ofisi ya madini, ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa