Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kujifanyia tathmini sababu za kupata hati yenye mashaka kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na kuchukua hatua za kujisahihisha ili hali hiyo isijirudie tena.
Mheshimiwa Hapi ametoa kauli hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kilichofanyika leo tarehe 12 Julai, 2022 katika ukumbi wa Kanisa Katoliki eneo la Mgango.
“Halmashauri hii ilikuwa inapata hati safi kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017, sasa tujitathmini kuangalia ni wapi tumejikwaa, kwa nini tumepata hati isiyoridhisha na kuchukua hatua stahiki kusahihisha hali hii” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameitaka Halmashauri hiyo kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vikundi mbalimbali vilivyokopa mikopo ya Halmashauri hiyo ambavyo vilikuwa havijarejesha shilingi milioni 400 za Halmashauri.
Mkuu wa Mkoa ameitaka Halmashauri hiyo kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ili iweze kufikia asilimia 100 ikiwa ni pamoja na kununua mashine za kukusanya mapato (POS) ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri hiyo.
“Hata hivyo ninawapongeza kwa kuweza kupandisha makusanyo ya mapato ya Halmashauri kutoka asilimia 71 iliyokuwepo hadi asilimia 86 iliyopo sasa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kumuongezea uwezo Mkaguzi wa Ndani ili aweze kubaini matatizo yanapojitokeza ili kupunguza hoja za CAG katika Halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Musoma kufuatilia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo iliagiza Halmashauri hiyo ijenge zahanati mbili kwa kutumia mapato yake ya ndani.
Mheshimiwa Hapi ameiagiza Halmashauri hiyo kuzifanyia kazi hoja zote za CAG na kutoa taarifa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ndani ya mwezi mmoja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mheshimiwa Charles Magoma Nyambita ameeleza kuwa katika ukaguzi wa mwaka wa fedha 2021/2022 Idara ya Uhasibu ya Halmashauri hiyo ilisababisha Halmashauri hiyo kupata hati isiyoridhisha.
“Ninaomba nikueleze masikitiko yetu sisi madiwani wa Halmashauri hii kuwa hati chafu ilisababishwa kwa makusudi na uzembe baada yawahasibu kushindwa kufunga hesabu kama walivyokuwa wanatakiwa” alisema Mheshimiwa Nyambita.
Hata hivyo Msheshimiwa Nyambita ameeleza kuwa Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu wa Halmashauri hiyo aliyesababisha Halmashauri hiyo kupata hati isiyoridhisha amehamishwa na serikali kwenda katika Halmashauri nyingine.
“Miaka yote ya nyuma Halmashauri hii ilikuwa inapata hati safi isiyo na mashaka lakini mwaka huu Halmashauri imepata hati yenye mashaka kutokana na wahasibu wetu kutokufunga hesabu za Halmashauri inavyotakiwa” alisema Mheshimiwa Nyambita.
Mheshimiwa Nyambita ameeleza kuwa katika kipindi hiki, Halmashauri hiyo imepata fedha nyingi za miradi ya maendeleo na ameahidi yeye pamoja na Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo watajitahidi kuimarisha usimamizi wa miradi hiyo kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Khalfan Haule ameeleza kuwa Wilaya ya Musoma imeanza kuchukua hatua kuhakikisha fedha za mapato ya ndani zinakusanywa na matumizi ya Halmashauri yanasimamiwa vizuri.
“Tunakushukuru sana Mkuu wa Mkoa kwa usimamizi wako wa karibu, kwa sasa Halmashauri hii imeanza kufanyakazi vizuri na tunakuahidi kuendelea kusimamia ili kuongeza mapato ya Halmashauri” alisema Dkt. Haule.
Dkt. Haule ameeleza kuwa kwa sasa Halmashauri hiyo imebadilisha baadhi ya wakusanya ushuru, kuwafungulia mashtaka baadhi ya watu waliokuwa na fedha za Halmashauri pamoja na kuboresha usimamizi wa matumizi ya Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ilikuwa ina jumla ya hoja 90 na maagizo mawili ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na kati ya hoja hizo hoja za nyuma zilikuwa 50 na hoja za mwaka unaoishia Juni 30, 2021 ni 40. Hata hivyo baada ya kuwasilisha majibu ya Halmashauri kwa CAG, hoja 44 zimefungwa, hoja 04 zimepitwa na wakati, hoja 09 zimeondolewa zitakaguliwa wakati ujao wakati hoja 01 haijatekelezwa.
Aidha katika maagizo yaliyotolewa na LAAC, agizo moja limetekelezwa na agizo moja limepitwa na wakati huku Halmashauri hiyo ikipata hati safi kwa kipindi cha miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2016/2017 wakati mwaka 2020/2021 Halmashauri hiyo ilipata hati yenye mashaka.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Kamati ya ulinzi ya Wilaya ya Musoma, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mwakilishi Mkazi wa CAG Mkoa wa Mara na Wakuu wa Vitengo na Idara za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa