Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameipongeza Benki ya NMB kwa msaada mkubwa uliyoitoa katika sekta za elimu na afya katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ametoa pongezi hizo wakati wa hafla fupi ya kupokea msaada huo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Buhare iliyopo katika Manispaa ya Musoma leo tarehe 16 Julai 2021.
“Nimetaarifiwa kuwa NMB wametoa msaada wa vitanda, madawati, mabati na vifaa vya hospitali wenye jumla ya shilingi 140,000 katika Mkoa wa Mara, asanteni sana” amesema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa msaada uliotolewa katika Mkoa wa Mara ni mabati 2,580, madawati 937, vitanda nane kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambavyo vimegawiwa katika wilaya zote za Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa msaada uliotolewa na Benki ya NMB katika hafla hiyo ni sehemu ya msaada kubwa ambao wameutoa katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa msaada huu unaendana na malengo ya Mkoa wa Mara na Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujumla ya kuboresha huduma za jamii kwa wananchi wa Tanzania na hususan sekta za afya na elimu.
Aidha ameiomba Benki ya NMB kuendelea kutoa misaada ya hali na mali pale inapohitajika ili kuinua maendeleo ya Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB Bwana Baraka Wenslaus ameeleza kuwa msaada uliotolewa ni sehemu ya fedha zaidi ya shilingi bilioni 2 ambazo zimetengwa na benki hiyo kama asilimia moja ya faida yake ya mwaka jana kwa ajili ya kuirudisha kwenye jamii.
“Mwaka jana Benki ya NMB ilipata faida ya shilingi bilioni 205 ambazo kwa mujibu wa sera za benki hiyo asilimia moja hurudishwa kwa jamii katika maeneo ya elimu, afya na elimu ya fedha na ujasiriamali kwa watanzania” ameeleza Bwana Wenslaus.
Ameeleza kuwa kwa Mkoa wa Mara wanamatumaini msaada walioutoa utaleta mabadiliko chanya na kuimarisha huduma za jamii katika sekta ya elimu na afya.
Katika hafla hiyo ya kupokea msaada, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Alfany Haule, Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara, Meya na Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, viongozi wa CCM, walimu na wanafunzi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa