Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 12 Julai, 2022 ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa kupata hati safi ya ukaguzi kwa hesabu za Mwaka 2020/2021 na kuitaka Halmashauri hiyo kuongeza nguvu katika usimamizi wa mapato na matumizi.
Mheshimiwa Hapi ametoa kauli hiyo wakati alipohudhuria kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2020/2021.
“Ninawapongeza sana kwa kupata hati safi lakini kutokana na taarifa hii ninataka Halmashauri iendelee kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi katika makusanyo ya mapato ya ndani” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha Mheshimiwa Hapi ameipongeza Manispaa ya Musoma kwa kufanya vizuri katika kusimamia makusanyo ya mapato ya ndani ambapo mpaka sasa Halmashauri hiyo ipo katika asilimia 104.
Mheshimiwa Hapi amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma kuhakikisha wakusanya mapato 47 ambao hawajasainiana mkataba na Manispaa hiyo kufanya hivyo haraka iwezekanavyo ili kuondoa uwezekano wa upotevu wa fedha za Halmashauri.
Aidha amemtaka Mkurugenzi kufuatilia suala la baadhi ya wananchi waliolipia lesseni ambao hawakukatiwa lesseni za biashara zao na vibanda vya Halmashauri ambavyo vimepangishwa bila kulipiwa kodi ya vibanda.
Mhehsimiwa Hapi amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma kuimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ili kiweze kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kuisaidia Halmashauri hiyo kubaini changamoto mbalimbali na kuziondoa kabla ya Wakaguzi wa Nje hawajaziandika.
Mheshimiwa Hapi ameitaka Halmashauri hiyo kukarabati magari chakavu ili yaweze kutumika na kufanya utaratibu wa kuyaondoa magari hayo katika vitabu vya Halmashauri.
Ameitaka taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kukamilisha uchunguzi na kupelewa suala la madai ya shilingi milioni 272 za Mkandarasi Norplan TZ Ltd mahakamani na kuvishirikisha vyombo vingine vya dola katika kuwatafuta viongozi wa VIMU Saccoss wanaodaiwa na Manispaa ya Musoma shilingi milioni 48 walizokopeshwa.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Musoma Mheshimiwa William Gumbo ameeleza kuwa Halmashauri itatekeleza maagizo yote ambayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo Mstahiki Meya ameeleza kuwa Manispaa hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ardhi ya akiba na hivyo kuwahitaji kulipa fidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayoanzishwa kutoa huduma kwa wananchi.
Ameeleza kuwa kuhusu mapato kukusanywa kinyume na sheria inatokana na wananchi kugomea kulipia baadhi ya huduma na ushuru kulingana na ilivyopangwa na Halmashauri hiyo na badala yake kulazimisha kulipia pungufu.
Manispaa ya Musoma ilikuwa na hoja 66 za ukaguzi ambamo kati yake kuna hoja za nyuma 22, hoja za mwaka 2020/2021 37 na maagizo 07 ya kikao cha Kamati ya Bunge la Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC). Aidha kati ya hoja hizo, hoja 22 zimefungwa wakati hoja 44 zinaendelea.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Kamati ya ulinzi ya Wilaya ya Musoma, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mwakilishi Mkazi wa CAG Mkoa wa Mara na Wakuu wa Vitengo na Idara za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa