Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 9 Novemba, 2021 ameanza ziara ya siku tatu katika Wilaya za Rorya, Tarime na Serengeti kukagua ujenzi wa miradi inayotokana na fedha za Mpango wa Maendeleo na Mapambano dhidi ya UVIKO 19.
Akiwa katika Wilaya ya Rorya amekagua ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi moja katika Shule ya Sekondari ya Suba na ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa na ofisi mbili katika Shule ya Sekondari ya Nyanthrogo.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Mheshimiwa Hapi ameutaka uongozi na watendaji wa Wilaya ya Rorya kujitathmini kuhusiana na maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo, upatikanaji na ubora wa vifaa vinavyopatikana katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Ninaomba viongozi na watendaji mjitathmini na kuona kama mpo katika njia sahihi ya kuelekea kukamilisha madarasa haya tarehe 1 Desemba 2021 kama tulivyokubaliana awali kwa ubora na kasi inayotakiwa kwa njia mnazozitumia” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewakumbusha kuwa badi siku 21 miradi hiyo inatakiwa ikamilike kulingana na makubaliano yaliyofanyika katika ngazi ya Mkoa kuhusiana na mkakati wa kutekeleza miradi hiyo.
Akiwa katika Shule ya Sekondari ya Suba ameshuhudia msingi kujengwa kwa mawe badala ya matofali kama ilivyokubalika katika kikao cha Mkoa na kazi haiendelei kwa sababu mafundi wamekosa vifaa muhimu ikiwa ni pamoja na simenti na mawe ili kuweza kufanya maandalizi ya kumwaga jamvi.
Aidha katika Shule ya Sekondari ya Nyanthorogo amekuta msingi umechimbwa haujaanza kujengwa huku matofali yanayotengenezwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo yakiwa yanamwagiliwa kwa maji yanayosombelewa kwenye madumu.
“Kwa kasi hii ya kufyatua tofali chache kwa siku, na umwagiliaji wa aina hii kuna wasiwasi wa kukamilisha mradi kwa wakati lakini pia ubora wa matofali na hatimaye jengo litakalojengwa hapa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kusimamia upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika kwa ujumla kulingana na maelekezo ya Serikali na mapema iwezekanavyo ili kurahisisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Hapi amemtaka Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Bwana Erick Mwita kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusiana na vifaa pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo ili itekelezwe kwa ubora unaotakiwa.
“Haiwezekani matofali ayafyatue mtu mwingine na ayamwagilie mtu mwingine, ikitokea yameharibika au yapo chini ya kiwango kila mtu atamlaumu mwenzake na hamna atakayekubali kubeba hasara hiyo, na sisi kama Serikali hatutakubali hasara hiyo, mtawajibika” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amewataka madiwani, wanasiasa na wananchi kuwaacha viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza miradi hiyo kwa namna wanavyoona inafaa bila kulazimisha fedha zibaki Rorya wakati hamna mafundi na vifaa vya kutosha vya kukamilisha miradi hiyo kwa ubora na kasi inayotakiwa.
Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuangalia uwezekano wa kununua tofali katika vikosi vya jeshi vilivyoko katika Mkoa wa Mara ili kuweza kupata tofali zenye ubora na kwa wakati unaotakiwa.
Aidha amewataka wanafunzi kusoma kwa bidi kwani Serikali ya Awamu ya Sita inaboresha miundombinu ya elimu na mishahara ya walimu kwa manufaa yao, hivyo waongeze juhudi katika masomo yao na nidhamu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mheshimiwa Juma Issa Chikoka amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa maelekezo yake na amewataka wajumbe wa Kamati ya Ufuatiliaji ya Wilaya kukutana leo jioni baada ya ziara ya Mkuu wa Mkoa ili kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“Kwa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa, Rorya tunatakiwa kwenda kwa kasi mara mbili zaidi ya ilivyokuwa hapo awali na kwa ubora unaotakiwa” alisema Mheshimiwa Chikoka.
Mheshimiwa Chikoka ameahidi kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati kuruhusu wanafunzi kuanza kidato cha kwanza kuanzia Januari 2022 kwa mujib wa ratiba.
Wilaya ya Rorya imepatiwa jumla ya vyumba vya madarasa 113 ambapo kati yake vyumba 98 ni vya Shule za Sekondari wakati madarasa 15 ni ya Shule Shikizi za Msingi kati ya vyumba ya madarasa zaidi ya 600 vilivyotengwa kwa ajili ya Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi tayari amewasili Tarime kwa ajili ya kuanza ziara yake kwa siku ya pili katika Wilaya ya Tarime hapo kesho.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa