Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 13 Julai, 2022 amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuunda tume ya uchunguzi kuhusu ujenzi wa Shule ya Sekondari ya katika Kata ya Binagi na kuwasilisha taarifa ndani ya wiki mbili.
Akizungumza katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa amepata taarifa kuwa fedha zilizoletwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo zimeisha na ujenzi haujakamilika.
“Serikali ilileta fedha kwa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya kata katika Kata ya Binagi na taarifa nilizonazo fedha zimeisha, ujenzi umesimama na haujakamilika, ninataka taarifa ndani ya wiki mbili” alisema Mheshimiwa Hapi.
Fedha za ujenzi wa Shule ya Binagi zinatokana na fedha za tozo ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ilipata fedha za kujenga shule mbili mpya katika Kata ya Binagi na Kata ya Sirari.
Aidha, Mheshimiwa Hapi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha inaongeza watumishi katika Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ili kuimarisha utendaji katika kitengo hicho.
“Halmashauri hii ina fedha nyingi na miradi mingi ya maendeleo haitakiwi kuwa na Mkaguzi wa Ndani mmoja tu ambaye pia ndiye Mkuu wa Kitengo, hii inasababisha mapungufu zaidi kwenye usimamizi wa fedha na miradi ya Halmashauri” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka madiwani wa Halmashauri hiyo kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha wataalamu hususan wahandisi wanafika katika miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Katika kikao hicho pia Mheshimiwa Hapi alitoa mrejesho wa maamuzi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kuhusiana na matumizi ya fedha za CSR zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bwana Solomon Shati ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imepata hati safi na kwa kipindi cha miaka sita mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2020/2021.
Hata hivyo Bwana Shati ameeleza kuwa Halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 98 na kati ya hoja hizo hoja za miaka ya nyuma 60 na hoja 38 ni za mwaka wa fedha 2020/2021 na maagizo mawili ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Bwana Shati ameeleza kuwa katika hoja zilizopita 60 za miaka ya nyuma, hoja 34 zimeshatekelezwa na kufungwa, hoja 18 zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji, hoja 02 zimejirudia huku hoja 06 hazijatekelezwa.
Aidha, Bwana Shati ameeleza kuwa kati ya hoja 38 mpya hoja 19 zimefungwa hoja 18 zipo kwenye utekelezaji na hoja moja ni hoja za kujirudia na kwamba Halmashauri hiyo imefanikiwa kufunga asilimia 54 ya hoja zote zilizotolewa na CAG.
Kikao cha Baraza la Madiwani Maalum kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kamati ya Ulinzi ya Mkoa na Wilaya ya Tarime, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Katibu Tawala wa Wilaya na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa