Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 18 Julai, 2022 amewakumbusha Wakuu wa Idara za Mipango kuzisaidia Halmashauri katika kufuatilia, kutekeleza na kusimamia vipaumbele vya Halmashauri likiwemo suala la lishe.
Akizungumza katika kikao cha kufanya tathmini ya utekelezaji wa Afua za Lishe katika Mkoa wa Mara kilichofanyika leo katika ukumbi wa Uwekezaji, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa bila ya Maafisa Mipango kutoa kipaumbele kwenye suala la lishe, utekelezaji wake unaweza kuwa mgumu.
“Mtu wa kuwakumbusha viongozi kuhusu masuala yote muhimu ya Halmashauri ni Mkuu wa Kitengo cha Mipango, akilala huyu Halmashauri yote inalala lakini akitimiza wajibu wake vizuri atawakumbusha viongozi na wahusika kuhusu majukumu muhimu ya Halmashauri ” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amewakumbusha Waweka hazina wa Halmashauri kulipa fedha zote zilizoidhinishwa na Wakurugenzi na kama kuna sababu ya kutokulipa Mwekahazina anatakiwa kumpa mrejesho Mkurugenzi au yoyote aliyetoa idhini ya malipo na sio kuamua tu yeye mwenyewe kulipa, kulipa pungufu au kutolipa kabisa.
Mheshimiwa Hapi ameagiza Waweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuwasilisha maelezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa kutokana na kutokulipa kiasi cha fedha kilichoidhinishwa na wakurugenzi wao kwa ajili ya kutekeleza Afua za Lishe.
Aidha amemuagiza Mkurugenzi wa Mji wa Bunda kumpangia majukumu mengine Afisa Lishe wa Halmashauri hiyo ambaye amesababisha Halmashauri kushindwa kutumia fedha zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya Afua za Lishe katika Halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Hapi amechukua hatua hizo kutokana na baadhi ya Halmashauri kufanya vibaya katika viashiria vya utekelezaji wa Afua za Lishe kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Halmashauri kutokutoa kipaumbele katika utekelezaji wa suala la lishe kulingana na miongozo ya Serikali.
Mheshimiwa Hapi amezipongeza Halmashauri zilizofanya vizuri katika suala la kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Afua za Lishe ikiwa ni pamoja na Manispaa ya Musoma asilimia 98.07, Halmashauri ya Mji wa Tarime asilimia 84.86 na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime asilimia 83.12.
Aidha Halmashauri zilizofanya vibaya katika kipengele hicho ni Halmashauri ya Wilaya ya Bunda asilimia 6.64, Halmashauri ya Mji wa Bunda asilimia 26.26 na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama asilimia 28.52.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kuna madhara makubwa kwa serikali wananchi wakiwa hawana lishe bora kwa sababu Serikali inapoteza fedha nyingi kuhudumia wagonjwa ambao asilimia kubwa yanachangiwa na lishe duni.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Mkoa wa Mara Bwana Paul Makali ameeleza kuwa pamoja na juhudi mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali pamoja na wadau, bado suala la lishe ni muhimu sana kupewa kipaumbele ili kuondokana na madhara ya lishe duni.
Bwana Makali ameeleza kuwa waathirika wakubwa wa lishe duni ni Watoto chini ya umri wa miaka 5 ambao wasipopata lishe bora wapo katika hatari ya kudumaa.
“Kwa sasa Mkoa wa Mara una watoto chini ya miaka mitano wenye udumavu wapatao 132,000 ambao ni wengi na hatimaye Mkoa utakuwa na watu wengi ambao wanaudumavu katika kukua kwao jambo ambalo ni tatizo katika jamii” alisema Bwana Makali.
Bwana Makali amezitaka Halmashauri kuongeza mkazo kwenye utekelezaji wa Afua za Lishe hususan kwenye masuala ambayo hayahitaji fedha kama vile kutoa ushauri nasaha kwa akina mama wanaohudhuria kliniki, kugawa matone ya vitamin A na kadhalika.
Kikao cha tathmini ya Afua za lishe katika Mkoa wa Mara kilihudhuriwa pia na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara, Vitengo na baadhi ya wataalamu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Waweka Hazina, Wakuu wa Idara za Mipango, Waganga Wakuu na Maafisa Lishe wa Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa