Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo ametoa mkono wa pole kwa familia za wanafunzi wa kike sita wa Shule ya Msingi Ochuna, Wilaya ya Rorya waliofariki dunia wakiwa katika bwawa lenye tope katika Skimu ya Umwagiliaji ya Ochuna.
Akiwasilisha rambirambi hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mhe. Juma Chikoka amesema Mhe. Rais ameguswa na msiba huo na kutoa rambirambi ya shilingi milioni 30 kwa ajili ya familia za watoto sita waliopoteza maisha katika tukio hilo.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameguswa kama Rais, Mama na mlezi na anawapa pole wafiwa wote walioguswa na msiba huu, yupo pamoja nasi wananchi wa Rorya katika kipindi hiki cha maombolezo” amesema Mhe. Chikoka.
Mhe. Chikoka amesema Mhe. Rais ametoa shilingi milioni 5 kwa kila familia iliyopata msiba huo fedha ambazo zilikabidhiwa kwa wafiwa na Mhe. Chikoka baada ya kuzitembelea familia hizo kwenye makazi yao.
Akizungumza na wananchi waliokusanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Ochuna, Mhe. Chikoka amesema miili ya wanafunzi hao itaagwa rasmi Jumatano ya tarehe 28 Agosti, 2024 katika viwanja hivyo na baada ya hapo mazishi yatafanyika kulingana na taratibu zitakazokubaliwa na familia za marehemu.
Mhe. Chikoka pia amewataka wananchi hao kupokea salamu za pole kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na Mbunge wa Jimbo la Rorya Mhe. Jafari Chege ambao wapo nje ya Mkoa kikazi na watoa pole sana kufuatia msiba huo.
Mhe. Chikoka amesema Serikali itaratibu zoezi la kuaga miili hiyo na mazishi ikishirikiana na Mbunge wa Rorya Mhe. Chege na wadau wengine wa maendeleo na familia za wanafunzi hao.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ochuna Mwalimu Richard Gasper Mahe amesema wanafunzi waliofariki ni wa darasa la tatu, wawili, darasa la nne wawili na darasa la tano mmoja na darasa la sita mmoja na wote walikuwa marafiki na wengi wao walikuwa wanashika nafasi ya kwanza au ya pili katika ufaulu kwenye madarasa yao.
Mwalimu Mahe amewataja wanafunzi waliofariki kuwa ni Eliza Jackton Okumbe wa darasa la nne na mdogo wake Yunis Jackton Okumbe wa darasa la tatu, Suzana Chacha Mwita darasa la tatu, Evaline Emmanuel Sylvanus darasa la sita, Anjerina Josepha Suke darasa la tano na Pendo Emmanuel Nyasanda darasa na nne.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ochuna Bwana Erick Nyagandi amesema chanzo cha tukio hilo ni mtoto mmoja aliyekuwa akikimbizana na bata majini na kujikuta kwenye kina kirefu chenye tope na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada na wenzake kwenda kumuokoa na kujikuta wanazama hadi kufika sita.
Bwana Nyagandi amesema kulikuwa na watoto saba katika eneo hilo na mmoja aliogopa kuingia baada ya kuona wenzake wamezama ndio aliyetoa taarifa kuhusu wenzake waliozama kwa wananchi ambapo walipoenda kuwaokoa walikuwa wakiwa tayari wamekufa.
Bwana Nyagandi amesema awali mwaka 2004 watoto wengine wawili wakike walizama na kufariki dunia katika bwawa hilo na hivyo kuweka jumla ya watoto nane wakike tangu bwawa hilo lijengwe.
Bwana Nyagandi amesema uongozi wa Kijiji hicho umependekeza watoto hao baada ya kuagwa wazikwe eneo moja kwa sababu walikuwa ni majirani na marafiki wakati wa uhai wao na ili kutoa fursa kwa wananchi wa eneo hilo kushiriki mazishi ya watoto hao.
Bwana Nyagandi amemshukuru Dkt. Samia kwa kutoa mkono wa pole kwa familia zilizofikwa na tukio hilo na kumuomba aendelee na moyo huo katika kuwajali wananchi wa Tanzania na hususan wanaopitia katika kipindi kigumu katika maisha yao.
Mkuu wa Wilaya aliambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati Usalama Wilaya ya Rorya, Mkurugenzi wa Halmashauri, mwakilishi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Rorya pamoja na viongozi wa Tarafa, Kata na Kijiji wa eneo hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa