Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu leo tarehe 8 Julai, 2024 amefungua mafunzo ya Waratibu wa Mpango wa M-MAMA na Waratibu wa Elimu kwa Umma kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwembeni Complex Manispaa ya Musoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Masatu ameishukuru Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Pathfinder International na Vodaphone Foundation kwa kuandaa mafunzo hayo.
“Ninazishukuru pia namna Halmashauri zinavyoshirikiana na Mkoa katika kutekeleza Mpango wa M-MAMA na kuleta manufaa yaliyotarajiwa katika jamii” amesema Dkt. Masatu.
Dkt. Masatu amewataka washiriki kutekeleza makubaliano yaliyowekwa na yatakayowekwa na hususan katika mpango wa kuifikia jamii na kuieleza matumizi ya namba 115 wakati wa dharura za akina mama wajawazito na watoto wachanga.
Dkt. Masatu amewaagiza washiriki kuwasilisha taarifa kwa viongozi wao ili mpango wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa uanze bila kuchelewa.
Kwa upande wake, Mratibu wa M-MAMA kutoka Pathfinder International Bwana Julius Titus ameupongeza Mkoa wa Mara kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa mpango wa M-MAMA kitaifa na kufanikiwa kuwaingiza na kuwalipa madereva jamii kulingana na utaratibu wa mpango huo.
Bwana Titus amesema awali, malipo ya madereva jamii yalikuwa yakitolewa kawaida ambapo Mkoa wa Mara ulifanya vizuri lakini hata mfumo wa malipo ulipobadilishwa kuwa katika mfumo wa kielekroniki bado Mkoa wa Mara ulifanya vizuri.
Kutokana na kazi nzuri iliyoonekana, Mtaalamu wa TEHAMA wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Bwana Samwel Kuboya aliteuliwa kuwa sehemu ya wakufunzi wa mafunzo hayo kitaifa na ametumika pia katika kusaidia kuboresha mfumo mzima wa M-MAMA.
Aidha, Msimamizi wa Kituo cha M-MAMA katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Bwana Oscar Isage aliteuliwa kwenda kufundisha usimamizi wa vituo hivyo katika mikoa mingine.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mpango wa M-MAMA katika Mkoa wa Mara Bwana Stanley Kajuna amewataka waratibu wa M-MAMA na waratibu wa Elimu kwa umma wa Halmashauri kujifunza vizuri kuhusu mpango wa M-MAMA na kutoa elimu namna mpango huo unavyofanya kazi hapa nchini.
Bwana Kajuna amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kuhusu mfumo wa M-MAMA, kuwawezesha washiriki kuwa na ujuzi na uwezo wa kuhamasisha jamii katika mfumo wa M-MAMA kwa ufanisi na kutengeneza mpango kazi wa utekelezaji.
Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Jamii Bibi Sophia Kiwanga ameshukuru kwa Serikali kuandaa mafunzo hayo na kuwashirikisha Waratibu wa Elimu kwa Umma kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Bibi Sophia amewataka Waratibu hao kujiongeza na kufanya kazi kwa bidii na ubunifu huku wakishirikiana na maafisa wengine na hususan Maafisa Habari na Waratibu mbalimbali wa masuala ya afya katika Halmashauri zao.
Bibi Sophia amewataka Waratibu wa Elimu ya Afya kwenye Halmashauri kuboresha taarifa kwenye mfumo na kutoa elimu ya afya kwa umma mara kwa mara kwa kutumia redio za kijamii na mikutano ya elimu kwa umma.
Mkoa wa Mara ni sehemu ya mikoa sita ya Tanzania Bara iliyozindua rufaa za jamii kuanzia tarehe 1 Mei, 2023 ikitanguliwa na Mkoa wa Shinyanga ambao ulizindua mpango huo awamu ya kwanza kwa majaribio na sasa mpango huo umeshasambazwa nchi nzima.
Mpango wa M-MAMA unalenga kurahisisha usafiri wa wagonjwa katika jamii kwa kuwawezesha madereva katika jamii kuwapeleka wanawake wajawazito na watoto wachanga kwenda vituo vya kutolea huduma za afya kwa uharaka zaidi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa