Naibu Waziri wa Madini Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa amewataka wajumbe wa Nyabigena Mining Society Limited wanaodai fidia baada ya eneo lao la uchimbaji kuchukuliwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kuwasilisha vilelelezo vya madai hayo katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Kiruswa ametoa agizo hilo baada ya kufanya mazungumzo yaliyowahusisha viongozi wa Mkoa wa Mara, Wilaya ya Tarime, wabunge, madiwani na viongozi wa ushirika wa Nyabigena Mining Society Limited tarehe 6 Novemba, 2022 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Tarime kujadili mustakabali wa madai hayo.
“Ninatoa hadi tarehe 30 Novemba, 2022 vielelezo na Ushahidi wote uwasilishwe ili uweze kuhakikiwa na Serikali kwa ajili ya kujiridhisha kabla ya wanaodai kulipwa stahiki zao” alisema Dkt. Kiruswa.
Katika kikao hicho pia, Mheshimiwa Kiruswa amemtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hao na viongozi wa ngazi mbalimbali kuhusu taratibu zilizopo katika kupata haki zao katika madai ya fidia ya ardhi na mali nyingine zilizokuwepo.
Aidha, Dkt. Kiruswa amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara Apolinary Lyambiko kuwasilisha nyaraka na vielelezo vinavyoonyesha mikataba kati ya mgodi huo na Vijiji vitano vilivyoingia mkataba na mgodi huo ili kubaini nani alipaswa kuwalipa wananchi hao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele amemshukuru Naibu Waziri kwa kuweza kuja na kusikiliza wananchi hao wenye madai ya fidia na kupunguza malalamiko ya wananchi wa Wilaya ya Tarime.
Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Vijijini Mheshimiwa Mwita Waitara amewataka viongozi wa makundi ya wanaodai fidia kuungana wao kwa wao na kuwa na kauli moja katika madai yao ili kuweza kurahisisha kusikilizwa na madai yao kupatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Waitara amewataka walalamikaji kuwasilisha vielelezo vyao halali na kutoa taarifa kwa viongozi na Serikali kuhusu udanganyifu wowote unaoweza kutokea ili wapate haki yao.
Mheshimiwa Waitara amewataka wananchi hao kuwasilisha madai halali na kutoa taarifa zote muhimu ili wananchi wenye haki katika madai hayo waweze kulipwa fidia zao.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara Mhandisi Joseph Kumburu ameeleza kuwa tayari ofisi yake imemteua Afisa atakayepokea taarifa na vielelezo vyote katika Kituo kidogo cha kuuza madini katika eneo la Nyamongo Wilayani Tarime.
“Watu wote wenye madai wanaweza kuwasilisha vielelezo vya madai yao kwenye ofisi hiyo iliyopo Nyamongo kuanzia tarehe 7 Novemba, 2022 ili kuwarahisishia kufika kwa urahisi” alisema Mhandisi Kumburu.
Wachimbaji wa Nyabiguna Mining Society Limited 362 ndio walikuwa waanzilishi wa uchimbaji wa madini katika eneo hilo ambapo baadaye liliuzwa na vijiji vyao kwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara lakini katika kulipa fidia baadhi yao walilipwa wengine hawakulipwa kabisa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa