Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vicent Naano Anney amemuagiza Mtendaji wa Kata ya Nyamuswa na Mtendaji wa Kijiji cha Bukama kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya shheria viongozi wa kijiji cha Bukama na wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Bushore waliogoma kuchangia chakula cha watoto shuleni.
Mhe. Dkt. Anney ametoa maagizo hayo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mradi wa Project Zawadi na Diwani wa Kata hiyo wakilalamikia kitendo cha wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo kugoma kuchangia chakula cha watoto wao kwa madai kuwa wakichangia chakula hicho kitaibiwa na walimu.
“Ninaagiza kuanzia wiki ijayo, chakula kiwe kinatolewa katika shule hii, kama hakipo kamata viongozi wa kijiji na wote wanaokataa kuchangia chakula peleka polisi ili waende mahakamani, haiwezekani tunabembelezana katika masuala ya msingi kama chakula cha watoto shuleni” amesema Mhe. Dkt. Anney.
Mhe. Dkt. Anney amesema kuweka chakula shuleni sio hiari bali ni maelekezo ya Serikali na kuwataka wananchi wa Kijiji cha Bukama kuacha uzembe, uchoyo, roho mbaya na chokochoko zisizo na tija na badala yake kuchangia chakula kinachohitajika ili watoto wao waweze kusoma vizuri na kuweza kubadili matokeo ya shule hiyo.
Mhe. Anney amepongeza Shirika la Project Zawadi kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika kukuza elimu katika Tarafa ya Chamriho, Wilaya ya Bunda kwa kusaidia ujenzi wa miundombinu, mafunzo kwa walimu, mafunzo ya kilimo kwa wanafunzi na wanajamii na ufadhili kwa wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu.
Mhe. Dkt. Anney amemtaka Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda kuhakikisha Shirika hilo linaalikwa kwenye vikao vya tathmini ya Lishe katika Wilaya ya Bunda ili kuhakikisha kuwa shirika hilo linatambulika katika wadau muhimu wa maendeleo katika ngazi ya Wilaya na Mkoa.
Aidha, ameagiza shule zote za Wilaya ya Bunda kutumia maeneo ya shule angalau ekari tatu kwa ajili ya kilimo cha chakula cha wanafunzi ili kuongezea kwenye chakula kinachotolewa na wazazi wa wanafunzi na kuhakikisha shule zote watoto wanakula angalau mara moja kwa siku.
Akiwa katika eneo hilo pia, Mhe. Dkt. Anney amekemea imani za kishirikina kwa wanaopata ugonjwa wa kuharisha na kutapika badala ya kuzingatia kanuni za afya katika makazi yao, na kukemea unyanyasaji wa wanawake na watoto yatima kwa kuwanyanganya mali zao baada ya kufiwa na waume au wazazi wao.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Busore Victor Magaji Magaji amesema shule hiyo ilijengwa mwaka 1974 na kwa sasa ina wanafunzi 77 wa awali na wanafunzi 381 wa madarasa ya msingi na ina walimu nane na ilikuwa na nyumba tatu za walimu.
Mwalimu Magaji amesema changamoto kubwa inayoikumba shule hiyo ni wazazi wengi kukataa kuchangia chakula cha wanafunzi kwa kisingizio kuwa wakichanga kitaliwa na walimu wa shule hiyo jambo ambalo linaifanya shule hiyo kupata matokeo yasiyoridhisha.
Mwalimu Magaji amelishukuru Shirika la Project Zawadi kwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa shule hiyo wanaotoka katika mazingira magumu kwa kuwapatia mahitaji yote muhimu ya shule.
Katika taarifa yake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Project Zawadi Bi. Regina Mkama ameiomba Serikali kuwahamasisha wananchi kuchangia chakula shuleni ili watoto waweze kupata walau mlo mmoja ili kuboresha ufaulu wa wanafunzi na kuacha kuwatesa watoto kwa njaa wakiwa shuleni.
Bi. Mkama amesema walimu walikubali kuwaachia wawakilishi wa wazazi kusimamia suala la chakula cha wanafunzi lakini bado wazazi hawataki kuchangia ili watoto wale shuleni kama zilivyo katika shule nyingine za Wilaya ya Bunda.
Bi. Mkama amewashukuru wananchi waliojitolea katika miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika shule hiyo na kuwataka wasikatishwe tamaa na wenzao wanaopinga kushiriki katika miradi ya maendeleo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa