Ujenzi wa daraja la zege katika barabara ya Sirari Mwanza eneo la Nyamsangula wilayani Tarime ambapo kalavati lililokuwepo lililosombwa na maji umeanza na unategemea kukamilika baada ya wiki tatu.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima wakati akizungumza na wananchi katika eneo hilo leo tarehe 12 Aprili 2021.
“Awali kalavati lililokuwepo lilikuwa na kipenyo cha mita tano lakini sasa daraja linalojengwa litakuwa na vipenyo viwili vya mita tano kila moja ili kupitisha maji mengi zaidi” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa katika ajali hiyo ambayo ilitokea tarehe 11 Aprili 2021, watu watatu wamefariki dunia na maiti zao zimepatikana baada ya kusombwa na maji yaliyokuwa yamefurika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Malima amewapongeza wananchi kwa juhudi zao za kuweka daraja la muda ambalo litasaidia watoto kuvuka kwa ajili ya kwenda shule, hata hivyo ameiagiza TANROADS kuimarisha usalama wa daraja hilo la muda ili kunusuru maisha ya watu watakaokuwa wanavuka hapo.
Aidha Mheshimiwa Malima ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa jitihada kubwa zilizofanyika ili kurejesha mawasiliano katika barabara hiyo kwa haraka.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANROADS ameeleza kuwa ajali hiyo ilisababishwa na mvua kubwa zilizokuwa zinaendelea kunyesha ambazo zilisomba kipande kikubwa cha bati lililoziba maji yaliyokuwa yanapita katika calvati hiyo na kusababisha mafuriko.
Mhandisi huyo ameeleza kuwa kwa sasa magari yote yanayoenda na kutoka Kenya yanapita katikati ya mji wa Tarime wakati daraja hilo linapoendelea kujengwa.
Tayari mkandarasi yupo eneo la tukio na ameanza kazi ya kujenga daraja hilo ikiwa ni pamoja na kuweka daraja la muda ili wananchi waweze kupita.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa