Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mhe. Juma Chikoka amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara katika mapokezi ya washiriki wa mashindano ya Miss Lake Zone, 2024 na kuwataka washiriki hao kuvitangaza vivutio vya utalii vya Kanda ya Ziwa.
Mhe. Chikoka ametoa wito huo katika mapokezi ya washiriki hao yaliyofanyika katika hoteli ya Le Grand Beach baada ya kuhitimisha ziara ya siku nne ambapo washiriki hao walitembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika Mkoa wa Mara.
“Mikoa ya Kanda ya Ziwa ina vivutio vingi vya utalii vinavyotokana na uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ziwa Victoria na hifadhi nyingine na vivutio vya asili vya utalii ambavyo Watanzania wanapaswa kuvijua na kuvitembelea” amesema Mhe. Chikoka.
Mhe. Chikoka amesema Watanzania walio wengi wanapaswa kuhamasishwa kufanya utalii wa ndani katika vivutio vilivyopo Kanda ya Ziwa inayounganisha Mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita na Kagera.
Aidha, amewapongeza washiriki hao kwa kuutembelea Mkoa wa Mara ambao unamiliki Zaidi ya asilimia 75 ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, sehemu kubwa ya Ziwa Victoria na umebarikiwa kuwa na madini mengi na kuvutia wawekezaji wa madini katika kila Wilaya.
Mhe. Chikoka amewataka washiriki wote kuzingatia kauli mbiu ya mashindano hayo Urembo na Uongozi kwa kufuata mwenendo mzuri unaozingatia maadili, kujituma na unyenyekevu ili kuweza kufika mbali katika maisha yao.
Amewatolea mfano wa waliokuwa wasanii katika fani mbalimbali ambao kwa sasa ni viongozi mahiri wakutegemewa katika Taifa mfano Jokate Mwongero na Mwana FA ambao kwa sasa wanaweza kuwatumia kama mfano bora wa kuigwa.
“Mimi pia nilitoka kwenye Sanaa lakini kutokana na kazi nzuri, unyenyekevu na maisha niliyoishi, nikateuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya, ninajua hata ninyi mkijitahidi inawezekana” amesema mhe. Chikoka.
Kwa upande wake Meneja wa Le Grand Victoria Hotel Bwana Paul Mutinda amewataka washiriki hao kutumia ubunifu katika kuutangaza utalii wa ndani kwa Watanzania ili kuwavutia watu wengi Zaidi kutembelea vivutio vya utalii.
Bwana Mutinda amesema urembo ni fani inayohitaji ubunifu na kuwataka washiriki hao kuwa wabunifu katika fani hiyo ili kuweza kunufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na kushiriki katika tasnia hiyo.
Kwa upande wake, mwandaaji wa mashindano hayo Bi. Rosemary Selemani Range amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Afred Mtambi kwa kuwasaidia washiriki hao kuweza kufanya ziara ya siku nne katika Mkoa wa Mara kutembelea vivutio vya utalii.
Bibi Range ameeleza kuwa fainali za mashindano hayo zinategemewa kufanyika tarehe 31 Agosti, 2024 katika Hoteli ya Malaika Beach iliyopo katika Mkoa wa Mwanza na kuwakaribisha wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Mikoa jirani kushiriki katika hafla hiyo.
Amesema kama waandaji wa mashindano hayo, watayafanyia kazi maoni ya wadau kuhusiana na mashindano hayo na kuyaboresha Zaidi kadiri siku zinavyoenda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa