Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ashatu Hussein Kijaji Kachambwa leo amezindua chanjo ya mifugo katika Mkoa wa Mara katika vijiji vya Mariwanda na Sarakwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kuwataka wafugaji kuchangamkia fursa hiyo kuchanja na kuitambua mifugo yao kwa kuwa manufaa yake ni makubwa.
Akizungumza kwa nyakati tofauti Mhe. Ashatu amesema baada ya mifugo kuchanjwa na kutambuliwa, Tanzania itaongeza zaidi wigo wa kuuza nyama na mifugo nje ya nchi jambo ambalo litawahakikishia wafugaji soko la uhakika la kimataifa.
“Tayari nchi ya China imetuhakikishia kuhitaji nyama ya ng’ombe tani milioni 54, kuna fursa pia katika nchi za Ulaya na nchi tano za uarabuni mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya kupeleka wanyama kutoka Tanzania wakiwa hai” amesema Mhe. Ashatu.
Mhe. Ashatu amesema baada ya mifugo kutambuliwa itawasaidia wafugaji kuikatia mifugo yao bima na kuwawezesha kutumia mifugo yao kama dhamana ili kupata mikopo katika taasisi za kifedha ili kuweza kupata maendeleo zaidi.
“Awali ilikuwa haiwezekani kuikatia mifugo bima wala kutumia kama dhamana kupata mikopo lakini sasa inaenda kuwezekana na wafugaji wataweza kuzuia hasara ya mifugo yao kwa kuwa itakuwa imekatiwa bima” amesema Dkt. Ashatu.
Dkt. Ashatu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoimarisha ushirikiano wa kimataifa unaoiwezesha nchi kufanya biashara mbalimbali na kueleza kuwa kabla hajaingia madarakani Tanzania ilikuwa inauza nje ya anchi tani 1,000 tu lakini kwa sasa inauza tani 14,900.
“Baada ya kampeni hii kitaifa, nchi itaruhusiwa kusafirisha nyama na mifugo hai katika nchi yoyote ile duniani na kuiwezesha bei ya nyama na mifugo ya Tanzania kupanda na hivyo kuwanufaisha zaidi wafugaji wa Tanzania” amesema Dkt. Ashatu na kutokana na umuhimu wake Serikali inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 200 kufanya maboresha katika sekta ya mifugo kwa kipindi cha miaka mitano.
Aidha, Dkt. Ashatu amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kuanzisha kampeni ya Nyamachoma festival na kuigwa na mikoa mingine ambayo inaongeza soko la uhakika la mifugo ya Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mhe. Waziri amewahakikishia wananchi kuwa chanjo, alama za utambuzi, pikipiki kwa ajili ya maafisa watakaohusika na uhamasishaji wa chanjo hiyo zimeshafika Mkoa wa Mara na kampeni ya chanjo ya mifugo inategemewa kuendelea katika Mkoa wa Mara kwa muda wa miezi miwili kuanzia sasa.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Waziri, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi amesema shughuli kubwa za uchumi katika Mkoa wa Mara ni pamoja na ufugaji na Mkoa una mifugo mingi na wafugaji wake wanafuga katika maeneo yao na sio ufugaji wa kuhamahama.
Mhe. Mtambi amesema wafugaji wa Mkoa wa Mara wanaishukuru Serikali kwa kutoa chanjo na utambuzi wa mifugo zoezi ambalo amesema litaenda kubadilisha ufugaji wao na kuwahamasisha kufuga ufugaji wa kisasa.
Mhe. Mtambi amewapongeza wafugaji wa Kata ya Hunyari kwa kazi kubwa wanayoifanya katika ufugaji wa mifugo mbalimbali na kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika mipango mbalimbali ikiwemo kushiriki kikamilifu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini Mhe. Boniface Mwita Getere amemshukuru Mhe. Waziri kwa kufanya uzinduzi wa chanjo ya mifugo katika eneo hilo na kuongeza kuwa yeye pia ni mfugaji wa eneo hilo na wanachangamoto kubwa ya umeme na maji.
Mhe. Getere amesema jitihada mbalimbali zimefanyika kutatua changamoto hiyo lakini bado mahitaji yao ni makubwa na wakiweza kupatiwa huduma za umeme na maji wanaweza kufuga kibiashara zaidi katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania Bwana Mrida Mshoda amesema wafugaji wa wanaishukuru sana Serikali kwa sababu ruzuku inayotolewa ambayo amesema itawanufaisha wafugaji kwa kuitambua na kuikinga mifugo yao.
Bwana Mshoda amesema awali, wafugaji wengi kutokana na gharama walikuwa hawachanji mifugo yote n ahata wakifanya hivyo walikuwa wanasubiri hadi kuwe na ugonjwa au ianze kuugua jambo ambalo mara nyingi lilikuwa linawasababishia hasara kubwa kutokana na mifugo hiyo kufa.
Aidha, Bwana Mshoda ameomba Serikali kuwapatia ufumbuzi wa changamoto ya umeme kwa kuwa nyumba za wananchi zipo mbalimbali, marisho ya mifugo na maji ya kunyweshea mifugo katika eneo hilo ambalo uchumi wake kwa kiasi kikubwa unategemea ufugaji.
Katika hafla hiyo, Mhe. Waziri alipewa zawadi ya ng’ombe zaidi ya 10 kutoka kwa wafugaji mbalimbali waliokuwepo katika hafla hiyo na uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Bunda, Maafisa Kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na wafugaji.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa