Kamati ya siasa ya Mkoa wa Mara imeipongeza Shule ya Sekondari ya Nyanduga kutokana na ufaulu wa wanafunzi katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2021.
Akizungumza wakati wa kutembelea mradi wa maabara ya somo la biolojia katika shule hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye ameeleza kuwa shule hiyo imekuwa inafanya vizuri kwa muda mrefu na mara nyingi amekuwa akiwapatia zawadi kwa sababu ya ufaulu.
“Mimi kwa muda mrefu tangu nikiwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya nimekuwa nikiwapa ng’ombe na kilo 200 za mchele ili kuwahamasisha wanafunzi wafanye vizuri zaidi” alisema Mheshimiwa Kiboye.
Aidha ameipongeza shule hiyo kwa matokeo mazuri waliyoyapata na kuwahamasisha wanafunzi kukazana kusoma kwani walimu wa shule hiyo wanaonekana kuwa wapo vizuri katika ufundishaji.
Wakati huo huo Mheshimiwa Kiboye ametoa ng’ombe mmoja, mchele kilo 200 na maharage kilo 40 na kuahidi kukabidhi vitu hivyo tarehe 25 Julai 2021 asubuhi ili wanafunzi wa shule hiyo waweze kusherekea matokeo mazuri ya wenzao wa kidato cha sita.
Katika kuunga mkono sherehe hiyo Mbunge wa Rorya ameahidi kutoa Kuku 20, mbuzi watatu na kukamilisha darasa moja lililoanza kujengwa katika shule hiyo.
Aidha Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Rorya ameahidi kutoa mafuta ya kupikia na maji katoni 50 kwa ajili ya sherehe hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Ally Salum Hapi ameahidi kutoa shilingi 1,500,000 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za ukamilishaji wa darasa hilo na kuahidi kuwa Mkoa utatoa shilingi 100,000 kwa kila mwalimu wa shule hiyo aliyesababisha matokeo hayo.
Katika matokeo ya kidato cha sita Shule ya Sekondari ya Nyanduga ilipata ufaulu wa daraja la kwanza wanafunzi 20 daraja la pili wanafunzi 39 na daraja la tatu wanafunzi watano huku kukiwa hamna daraja la nne na sifuri katika shule hiyo ambayo ni ya serikali.
Katika matokeo hayo Mkoa wa Mara ulifanya vizuri na kushika nafasi ya tatu kitaifa huku Shule ya Sekondari ya Natta ambayo ni ya serikali iliyopo katika Wilaya ya Serengeti ikishika nafasi ya kwanza kimkoa katika ufaulu na kuingia katika shule 20 bora kitaifa katika matokeo hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa