Halmashauri ya Wilaya ya Butiama imempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi kwa kuiwezesha Halmashauri hiyo kupata ushuru wa huduma (service levy) kutoka kwa makampuni mbalimbali.
Akizungumza leo tarehe 15 Julai, 2022 katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Butiama Mheshimiwa Peter Wanzagi amesema kutokana na maagizo na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya ushuru wa huduma kutoka kwa migodi ya madini, wakandarasi wa barabara na wachimbaji wadogo wa madini.
“Kwa mwaka 2021/2022 Halmshauri imekusanya makusanyo ya ndani ya kutosha kutokana na maelekezo yako ambayo uliyatoa awali na sasa Halmashauri inafaidia nayo. Alisema Mheshimiwa Wanzagi.
Aidha, madiwani wa Halmashauri hiyo walimpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha za kukamilisha jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama iliyokuwa imesimama kwa muda mrefu na sasa linaendelea kukamilishwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa CAG wa mwaka 2020/2021.
Aidha, ameielekeza Halmashauri hiyo kuongeza juhudi kwenye makusanyo ya mapato ya ndani, kubana matumizi na kupunguza hoja za CAG.
Mheshimiwa Hapi ameitaka Halmashauri hiyo kufunga mfumo wa kukusanya mapato katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya ili kuiwezesha Halmashauri kupata mapato zaidi katika eneo hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Bibi Patricia Robi Kabaka ameeleza kuwa Halmashauri hiyo ilipata hati safi ya ukaguzi katika mwaka wa fedha 2020/2021.
Hata hiyo Bibi Kabaka ameeleza kuwa katika ukaguzi huo, Halmashauri ina jumla ya hoja 65 na kati ya hizo, hoja 47 ni za miaka ya nyuma na hoja 18 ni za mwaka 2020/2021.
Bibi Kabaka ameeleza kuwa kati ya hoja hizo, hoja zilizofungwa 30, hoja zilizopo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, hoja 03 hazijatekelezwa, hoja 01 imepitwa na wakati, hoja 04 zinajirudia.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa