Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mwalimu Lyidia Bupilipili ameiomba Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMESEMI) inapogawa upya halmashauri za Wilaya ya Bunda kuzingatia suala la upatikanaji wa huduma kiurahisi kwa wananchi.
Mheshimiwa Bupilipili ameeleza hayo leo tarehe 22 Aprili wakati wa ziara ya Katibu Mkuu TAMISEMI Eng. Nyamhanga katika Wilaya ya Bunda.
“Ofisi yangu inapendekeza kuwa Halmashauri ya Mji wa Bunda iwe na Tarafa mbili za Serengeti na Chamliho na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda iwe na tarafa mbili za Kenkombyo na Nansimo ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma” alisema Mwalimu Bupilipili.
Ameeleza kuwa kwa sasa Wilaya hiyo ina tarafa nne ambapo Halmashauri ya Mji wa Bunda ina tarafa moja wakati Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ina tarafa tatu ambapo mbili zipo upande mmoja wakati nyingine ipo upande mwingine wa wilaya na hivyo kuwalazimisha wananchi kuvuka mji wa Bunda ili kwenda kupata huduma ilipohamia Halmashauri ya Wilaya upande mwingine ambako ni mbali.
Mheshimiwa Bupilipili ameeleza kuwa ofisi yake imependekeza kuwa ofisi za makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda yajengwe Kibara kama ilivyopendekezwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo na mapendekezo hayo tayari yamewasilishwa TAMISEMI.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mwalimu Amos J. Kusaja alisema Halmashauri ilipokea agizo la kuhamishia ofisi zake kwenye maeneo yao ya utawala na Baraza la Madiwani waliamua kuhamishia ofisi katika mji wa Kibara ambako wako hadi sasa.
Bwana Kusaja alisema Baraza la Madiwani liliamua Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ijengwe katika Tarafa ya Chamliho na Menejimenti ya Halmashauri ilipendekeza kuwa kutokana na hilo, ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Bunda zijengwe katika kijiji cha Makongoro jirani na hospitali ya wilaya mapendekezo ambayo hayakupitishwa na Baraza la Madiwani.
“Baada ya maamuzi ya madiwani, sisi katika menejimenti hatuna tena suala lingine tunasubiria maamuzi ya TAMISEMI na viongozi wengine” alisema Bwana Kusaja.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema TAMISEMI hufanya maamuzi yake kutegemea mapendekezo yaliyopokelewa na hususan maamuzi ya Baraza la Madiwani ambayo ni ya kisheria.
“Yaleteni tena mapendekezo hayo tuyaangalie vizuri, ili yaweze kufanyiwa kazi mara moja” alisema Eng. Nyamhanga.
Katibu Mkuu TAMISEMI alikuwa na ziara ya siku tatu katika Wilaya ya Tarime, Serengeti na Bunda katika Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 20 Aprili 2020 hadi tarehe 22 Aprili 2020.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa