Timu ya michezo ya Biashara United imepata udhamini wa uhakika kutoka katika mgodi wa North Mara na kiwanda cha Jambo Jamakaya wenye thamani ya shilingi milioni 450.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo tarehe 11 Septemba 2020, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amesema udhamini huu unatokana na timu kufanya vizuri katika ligi ya mpira kwa msimu wa mwaka 2019/2020.
“Msimu uliopita ligi yetu imefanya vizuri sana na tunategemea kwa ufadhili huu tutafanya vizuri zaidi katika mashindano ya msimu huu” alisema Mheshimiwa Malima ambaye pia ni Mlezi wa timu hiyo.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa Mgodi wa North Mara umetoa udhamini wa shilingi milioni 350 wakati kiwanda cha Jambo kimetoa udhamini wa takribani milioni 100.
“Hata hivyo bado tutahitaji wananchi waweze kuchangia shilingi milioni 150 iliyobakia katika makadirio ya timu ya milioni 600 ili timu iwe katika hali nzuri zaidi”
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Malima, wachezaji wameahidi kumaliza ligi wakiwa kati ya timu tano bora, jambo ambalo kutokana na uwekezaji huu anaamini linawezekana.
Aidha Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa ili kuboresha mazingira ya michezo Mkoani Mara, ofisi yake inaendelea na mazungumzo na Chama cha Mapinduzi ili kuweza kuboresha uwanja wa Karume ambao unatumiwa na timu ya Biashara United kama uwanja wao wa nyumbani.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa