Timu ya Biashara United iliyocheza Ligi Daraja la Kwanza iliyopo Mkoani Mara leo imekabidhiwa kwa mwekezaji mpya Free Sports Limited ili aweze kuiendeleza timu hiyo baada ya viongozi na wanachama Biashara United kushindwa kuiendesha.
Akizungumza baada ya kushuhudia makabidhiano hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu ameeleza kuwa makabidhiano hayo yanafungua ukurasa mpya kwa timu hiyo.
Bwana Makungu ameelezea kufurahishwa na makubaliano yaliyofikiwa baina ya Biashara United na mwakilishi wa Free Sports Limited na kuhitimishwa na makabidhiano yaliyofanyika mbele ya viongozi wa Mkoa wa Mara.
“Ni matumaini yangu, wananchi wa Mkoa wa Mara na hususan wapenzi wa soka wataunga mkono makubaliano yaliyofikiwa na kuendelea kuisaidia timu ya Biashara United” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mkoa wa Mara ameahidi kutoa ushirikiano kwa Timu hiyo na mwekezaji mpya na kutoa ushauri pale utakapohitajika.
Akizungumza baada ya kukabidhi timu hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Klabu ya Biashara United Bwana Agustine Mgendi ameeleza kuwa wanashukuru sana kupata mwekezaji wa kuendelea na timu hiyo.
“Tumemtafuta mwekezaji kwa muda mrefu, tunashukuru sasa amepatikana na ataiendeleza timu na kutoa fursa kwa vijana na watanzania kwa ujumla kupitia klabu hiyo” amesema Mgendi.
Aidha, Bwana Mgendi ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Mara kwa kuratibu makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na kushuhudia makabidhiano ya Timu hiyo kwa mwekezaji mpya.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Free Sports Limited Bwana Masau Bwire amesema kuanzia sasa mwekezaji atahakikisha kuwa timu hiyo inafanya vizuri na inapanda daraja ndani ya muda mfupi ili iweze kurudi kwenye Ligi Kuu ya Tanzania.
“Tutahakikisha kuwa ndani ya muda mfupi ujao, Biashara United itaingia Ligi Kuu na kushika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi kama ilivyokuwa katika kipindi cha 2021/2022” amesema Bwana Bwire.
Bwana Bwire amewaomba wananchi wa Mkoa wa Mara kuendelea kuiunga mkono na kuishangilia kwani bado itaendelea kuwepo katika Mkoa wa Mara.
Bwana Bwire ameeleza kuwa awali, Kampuni hiyo ilikuwa inaisaidia timu kulipa gharama mbalimbali ikiwemo mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi, usafiri, malazi na chakula.
Aidha, Bwana Bwire ameushukuru sana uongozi wa Mkoa kwa kusimamia makubaliano na kushuhudia makabidhiano ya timu hiyo yanafanyika kwa maridhiano ya pande zote.
Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Menejimenti ya Mkoa wa Mara, wadau wa michezo na viongozi na wawakilishi wa wanachama wa Klabu ya Biashara United.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa