Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa leo tarehe 10 Novemba, 2024 amezindua ofisi na kuongoza harambee ya ukamilishaji wa ofisi za Jimbo Katoliki Bunda na kuwataka wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Akizungumza wakati wa harambee hiyo, Mhe. Bashungwa amewataka wananchi kushiriki kikamilifu matukio mbalimbali ya uchaguzi ikiwemo kuhudhuria kamapeni za uchaguzi ili kuwatambua wanaogombea na sera zao kwani ni muhimu kuwajua kabla ya kufanya maamuzi ya kuwachagua viongozi.
“Tumepewa fursa ya kuwachagua viongozi watakaowatumikia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ninaomba kuwasihi muitumie vuzuri fursa hii na kuwachagua viongozi bora watakaoshirikiana na Serikali kuwaletea maendeleo” amesema Mhe. Bashungwa.
Mhe. Bashungwa amewataka wananchi kushiriki kikamilifu uchaguzi ili wasiwalaumu watu wengine kwa kuwachagulia viongozi watakaowaongoza na kuwataka kutumia vizuri fursa hii na kuwachagua viongozi wazuri na wapenda maendeleo.
Mhe. Bashungwa amemshukuru Askofu Mwasondole kwa kumualika kushiriki katika harambee hiyo ambapo yeye na wafanyakazi wa ofisi yake wameahidi kuchagia shilingi 62,700,000 kwa ajili ya ukamilishaji wa Jimbo Katoliki Bunda.
Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa kwa sasa Jimbo Katoliki la Bunda lina miaka 13 tu tangu lilipoanzishwa na limefanikiwa kufanya mambo mengi na ni matumaini yake kuwa litakapofikisha miaka 25 ya jubilee yake litakuwa limepiga hatua kubwa ya maendeleo.
Mhe. Bashungwa amewataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa na kuwaombea viongozi wa Serikali ili Mungu awalinde na awawezeshe kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya Watanzania wote.
Ametumia fursa hiyo kuelezea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Mara katika Sekta ya Ujenzi ikiwemo miradi ya barabara, madaraja, ukarabati wa uwanja wa undege wa Musoma na mzani wa Robanda, Wilaya ya Bunda unaopima magari yakiwa kwenye mwendo inayotekelezwa na Wakala wa Barabara (TANROADS).
Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa Serikali imekarabati vivuko vya MV Musoma na MV Mara na kujenga jengo la abiria katika eneo la Mwigobero, Manispaa ya Musoma na inampango wa kujenga jengo la kupumzikia abiria na kukarabati gati la kupaki vivuko katika eneo la Kinesi, Wilaya ya Rorya.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Vincent Naano Anney amewataka wananchi wa Bunda kushiriki kampeni za vyama vya siasa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kuwasikiliza na kuzielewa sera na mipango ya vyama hivyo.
“Vyama vitawanadi wagombea wake ambao wanagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi na hivyo niwasihi ndugu zangu tushiriki ili kupata uelewa wa wagombea na vyama vyao ili tuwachague tukiwa tunawaelewa” amesema Mhe. Dkt. Anney.
Aidha, Mhe. Anney ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda amewataka wananchi kushiriki uchaguzi tarehe 27 Novemba, 2024 ili kuweza kuwachagua viongozi bora watakaosimamia maendeleo katika maeneo yao.
“Tukiwachagua viongozi wazuri tutaachana na wale viongozi wababaishaji na wanaouza maeneo ya wananchi” amesema Dkt. Anney na kuongeza kuwa kumekuwa na viongozi wengi wanaochaguliwa na wananchi ambao wamekuwa chanzo cha migogoro katika jamii.
Mhe. Dkt. Anney amewasilisha ahadi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi shilingi milioni 3, Katibu Tawala Mkoa wa Mara shilingi 500,000 na ahadi yake yeye mwenyewe shilingi milioni moja na kuwasilisha ahadi za viongozi, watendaji wa Serikali na watu wengine aliowashirikisha kuhusiana na harambee hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa harambee hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda Simon Chibuga Masondole amemshukuru Waziri Bashungwa kwa kuweza kushiriki katika harambee hiyo na kueleze kuwa litakapokamilika jengo hilo litakuwa ni moja ya vivutio vya Mji wa Bunda.
Mhashamu Askofu ameeleza kuwa mpaka wakati huo tayari Jimbo Katoloki la Bunda lilikuwa limekusanya shilingi 62,700,000 ambazo ni michango ya waumini, parokia mbalimbali, vyama vya kitume na wahisani mbalimbali.
Askofu Masondole ameeleza kuwa katika kufanikisha harambee hiyo, Jimbo Katoliki Bunda liliomba mchango kutokana kwa marafiki mbalimbali ambao wamechangia shilingi 71,800,000 taslimu na ahadi ya shilingi milioni moja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Harambee, Jimbo Katoliki la Bunda Bwana Kulwa Kahabi ameeleza kuwa harambee hiyo ni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Jimbo Katoliki la Bunda ambayo ilianza mwaka 2022 na inatarajiwa kuhitimishwa mwaka huu.
Bwana Kahabi ameeleza kuwa mwaka 2022 walifanikiwa kukusanya shilingi milioni 240 ambazo zilitumika katika hatua za awali za ujenzi wa ofisi hizo; awamu ya pili ilikuwa mwaka 2023 ambapo walifanikiwa kukusanya shilingi milioni 130 ambazo zimesaidia katika ujenzi wa jengo hilo na kununua vifaa vya ofisi.
Bwana Kahabi ameeleza kuwa katika harambee ya wakati huu, Kanisa linategemea kukusanya shilingi milioni 350 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la ofisi hizo ili liweze kutoa huduma kwa waumini, watawa na wageni wanaotembelea Jimbo Katoliki la Bunda.
Katika harambee hiyo Jimbo Katokili la Bunda limefanikiwa kukusanya shilingi 272,657,150 na kati ya fedha hizo fedha taslimu shilingi 24,000,000; fedha zilizowekwa benki 169,227,650 na ahadi ni shilingi 20,230,000 pamoja na ahadi ya Mhe. Waziri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa