Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso (Mb.) anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yatakayofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 Septemba, 2021 katika Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela ameeleza hayo leo tarehe 10 Septemba 2021 wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa Kampeni ya Mkoa ya upandaji Miti kwa kila halmashauri; upandaji wa miti 10,000 na uwekaji wa vigingi 60 katika mipaka ya Bonde la Mto Mara katika vijiji vya Mrito na Kerende vilivyopo Wilayani Tarime” alisema Bwana Msovela.
Bwana Msovela ameeleza kuwa shughuli nyingine zitakazofanyika katika maadhimisho ya mwaka huu ni maonyesho ya wajasiriamali kutoka taasisi mbalimbali za umma na kijamii yatakayoanza tarehe 13 Septemba 2021 hadi tarehe 15 Septemba 2021 katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime.
Aidha maadhimisho hayo yatapambwa na michezo mbalimbali inayolenga kuhamasisha jamii kutunza na kuhifadhi vyanzo vya Bonde la Mto Mara kama vile kukimbiza kuku, mpira wa miguu, kukimbia kwenye magunia na kuvuta Kamba.
“Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mara kwa mwaka 2021 ni Tuhifadhi Mto Mara kwa Utalii na Uchumi Endelevu” alisema Bwana Msovela.
Bwana Msovela ameeleza kuwa Maadhimisho ya Siku ya Mara ni utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa kumi (10) wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria uliofanyika tarehe 04 Mei, 2012 katika mji wa Kigali nchini Rwanda ambao ulielekeza kufanyika kwa Maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day) kila mwaka tarehe 15 Septemba kuanzia mwaka 2012.
Bwana Msovela amewaalika wananchi wa Mkoa wa Mara, wafanyakazi, wajasiriamali, na wadau wote wa maendeleo ndani nan je ya Mkoa wa Mara kushiriki kwenye maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa