Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameendelea na ziara yake katika Wilaya ya Serengeti ambapo ametembelea Chuo cha Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) kinachooendelea kujengwa katika Kata ya Uwanja wa Ndege na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuacha kufanya tegesha inakwamisha maendeleo na kupandisha gharama za mradi wa maendeleo.
Mhe. Mtambi ametoa kauli hiyo baada ya baadhi ya wakazi wa eneo la Burunga kudai kuwa maeneo yao yamechukuliwa bila kufuata utaratibu na kujenga Chuo cha VETA na mpango wa Serikali kuhamisha barabara inayopita eneo hilo kupisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mugumu mambo ambayo yamethibitishwa katika kikao hicho kuwa sio kweli.
“Serikali haitamvumilia mtu yoyote anayekwamisha mradi wa maendeleo kwa ajili ya manufaa yake binafsi na tutamchukulia hatua mtu yoyote atakayefanya hivyo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Serengeti kufuatilia taarifa kuwa Wakala wa Barabaraa (TANROADS) Mkoa wa Mara iliwazuia wananchi hao kuendeleza maeneo yao kuanzia mwaka 2010 hadi sasa na tayari wameshafanyiwa tathmini tangu mwaka 2019.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Mateso Moses Kairo amesema awali, eneo hilo lilikuwa la Kijiji cha Burunga ekari 72 na Kijiji kiliamua kulitoa kwa Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA.
Bwana Kairo amesema kuwa baadaye baada ya mawasiliano na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, VETA ilipewa eneo la ekari 42 na ekari 10 walipewa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) na eneo lililobakia limekuwa ni mali ya kijij hicho.
Bwana Kairo amesema baada ya Serikali ya Kijiji kuvunjwa na eneo hilo kuingizwa kwenye Mamlaka ya Mji, baadhi ya wananchi wasiokuwa waaminifu walilivamia eneo hilo na kudai ni mali yao na wengine kuwauzia wageni waliokuwa wanatafuta maeneo.
Amesema kuwa wananchi waliovamia eneo hio walifungua kesi kwenye Baraza la Ardhi la Kata na Baraza la Ardhi la Wilaya ambapo wameshindwa lakini bado wakija viongozi maeneo hayo wanadai eneo hilo ni lao, vielelezo vya uhalali wa eneo hilo vipo na ndio vilipelekwa mahakamani.
Awali, wananchi wawili walijitokeza kudai fidia kutokana na maeneo yao kuchukuliwa kupisha mradi WA Chuo cha VETA na ujenzi wa barabara ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) jambo ambalo lilikuja kuthibitishwa katika kikao hicho kuwa sio sahihi.
Mkuu wa Mkoa amezungumza na wananchi waliokuwepo eneo la ujenzi wa Chuo cha VETA ambapo alitumia nafasi hiyo kusikiliza kero zao na kuzitolea ufafanuzi.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na baadhi ya Wajumbe wa Kamatiya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, Viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Mwenyekiti na Menejimenti ya Wilaya ya Serengeti na maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, taasisi na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa