Jumla ya wanafunzi 50,564 wanatarajiwa kufanya upimaji wa kitaifa wa Kidato cha Pili katika Mkoa wa Mara unaoanza leo tarehe 28 Oktoba, 2024 hadi tarehe 07 Novemba, 2024 kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga imeeleza kuwa kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 25,457 na wasichana ni 25,107 ambao wamo kwenye mikondo 1,309 katika shule za Sekondari 280 zilizopo katika Mkoa wa Mara.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ina shule 47 zenye watahiniwa 7,333, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ina shule 53 zenye watahiniwa 7,005, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ina shule 44 zenye watahiniwa 6,704 huku Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ikiwa na shule 31 zenye watahiniwa 6,101.
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ina shule 22 na watahiniwa 5,647, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ina shule 25 na watahiniwa 5,057, Manispaa ya Musoma ina shule 27 zenye watahiniwa 5,035, Halmashauri ya Mji wa Bunda ina shule 21 na watahiniwa 4,395 wakati Halmashauri ya Mji wa Tarime ina shule 16 na watahiniwa 3,287.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa maandalizi yote ya upimaji huo yamekamilika ikiwemo semina za wasimamizi wa upimaji na vifaa vya upimaji tayari vimeshasambazwa katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara.
Upimaji wa Kidato cha Pili unasimamiwa na Kamati za Uendeshaji za Mikoa/Halmashauri ambazo zimepewa mamlaka na Sheria ya Baraza la Mitihani sura 107 ya mwaka 1973 na marekebisho yake ya mwaka 2019.
Sekretarieti ya Mkoa wa Mara inawatakia wanafunzi wote wa Kidato cha Pili kila la kheri katika upimaji wa Taifa wa Kidato cha Pili.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa