Jumla ya watahiniwa 23,948 wanatarajiwa kufanya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne katika Mkoa wa Mara unaotegemewa kufanyika kuanzia leo tarehe 11 Novemba, 2024 hadi tarehe 29 Novemba, 2024 hapa nchini.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga imeeleza kuwa kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 12,617 na wasichana ni 11,331 ambao watafanya mtihani wakiwa kwenye mikondo 647.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa jumla ya shule za Sekondari 254 kutoka Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara zitahusika na mitihani hiyo ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ina shule 44, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti shule 43, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya shule 41, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma zenye shule 24 kila mmoja.
Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ina shule 23, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ina shule 22, Halmashauri ya Mji wa Bunda shule 19 na Halmashauri ya Mji wa Tarime shule 14.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa maandalizi kwa ajili ya ufanyikaji wa mitihani hiyo yameshakamilika na vifaa vya mitihani vimeshapokelewa na kusambazwa katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara.
Sekretarieti ya Mkoa wa Mara inawatakia kila la kheri wanafunzi wote wa Kidato cha Nne mwaka 2024 watakaofanya mtihani huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa