Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Paul Mhede amesema Serikali kwa kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) inategemea kuanza uzalishaji wa vifaranga vya samaki katika Mkoa wa Mara kuanzia Julai, 2025.
Dkt. Mhede ametoa kauli hiyo leo baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya Sekta ya Uvuvi katika mapokezi yake iliyofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji wakati wa kuanza kwa ziara yake ya siku mbili katika Mkoa wa Mara tarehe 20-21 Machi, 2025.
“Wizara ya Mifugo na Uvuvi itafuatilia kuona kuwa Mkoa wa Mara unapata vifaranga kwa ajili ya wafugaji wa samaki waliopo kupitia FETA na wauzaji binafsi wa vifaranga wa samaki” amesema Dkt. Mhede.
Dkt. Mhede amesema kupitia FETA iliyopo katika eneo la Gangimori, Wilaya ya Rorya, vifaranga vya samaki vitaanza kuzalishwa kuanzia mwezi Juni, 2025 na vifaranga hivyo vitauzwa kwa wananchi na taasisi kuanzia Julai, 2025 kwa wahitaji wa ndani nan je ya Mkoa wa Mara.
Dkt. Mhede ameipongeza Kampuni ya Godwin Lusaso General Supply Co. Limited kwa uwekezaji walioufanya na mpango wa kupanua uwekezaji huo na kuwahakikishia kuwa Serikali itawasaidia kupata mkopo mwingine katika taasisi ya fedha ili kuweza kupanua uwekezaji wao katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na kuanzisha kiwanda cha chakula cha samaki.
“Leteni andiko la mradi huo na Wizara itafuatilia marejesho kutoka TADB na italipeleka andiko hilo kwenye benki na taasisi nyingine za kifedha ili muweze kupata mkopo wa riba nafuu” amesema Dkt. Mhede na kuongeza kuwa kwa sasa mikopo inayotolewa kwa biashara za uvuvi riba zake zinajulikana kwa taasisi zote.
Dkt. Mhede amekiri kuna tatizo katika biashara ya chakula cha samaki na ameitaka Maabara ya Taifa ya Uvuvi (NFQCL) kupima ubora wa chakula cha samaki wanachouziwa wafugaji wa samaki katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kwa Upande wake, Afisa Uvuvi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Bi. Ghati Kisyeri amesema Mkoa wa Mara kwa kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na wadau mbalimbali umeendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kutumia fursa ya maji yaliyopo kuwekeza katika ufugaji wa samaki.
“Kwa sasa Mkoa una wafugaji wa samaki kwa njia ya visimba 39 wenye jumla ya visimba 241 vyenye ukubwa wa ujazo wa kati ta mita 40 hadi mita 1,600 vya plastiki na chuma na aina ya samaki wanaofugwa ni sato” amesema Bi. Kisyeri.
Bi. Kisyeri amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya wanufaika 19 ambao ni watu binafsi, vikundi, vyama vya ushirika wamepata mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) yenye thamani ya shilingi 1,227,350,000.
Amesema mbali na uwekezaji katika ufugaji wa samaki wa kisasa, Mkoa una mialo ya uvuvi 151 na wananchi 396,807 ambao wameajiriwa katika mnyororo wa sekta ya uvuvi kwa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Bi. Kisyeri amesema Mkoa wa Mara una wavuvi 17,093 na kati yao wavuvi wa nyavu ni 6,274, wavuvi wa dagaa ni 6,244, wavuvi wa ndoano ni 3,747 na wavuvi wengineo ni 799 na una wataalamu wa sekta ya uvuvi 42 na mahitaji ya wataalamu katika Halmashauri zote tisa ni 120 na una upungufu wa wataalamu 79.
Bi. Kisyeri amesema changamoto unaoikabili ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ni pamoja na kutokuwepo kwa mzalishaji wa chakula cha samaki chenye ubora, kutokuwepo kwa mzalishaji wa vifaranga, bei kubwa ya chakula cha samaki, kuongezeka kwa magugu maji ambayo huathiri maeneo yenye vizimba.
Aidha, amesema kuna changamoto kwa wafugaji wa samaki waliopokea mikopo ya riba nafuu kutokupata chakula cha kulisha samaki kwa wakati na chakula hicho hakipelekwi katika eneo la utekelezaji wa mradi kama ilivyokubalika katika mkataba.
Kwa upande wake, Bwana Joshua Mtei kutoka kampuni ya Godwin Lusaso General Supply Co. Ltd amesema kuwa kampuni hiyo imeanza kujishughulisha na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba Mei, 2024 wakiwa na vizimba vitatu na kwa sasa wanavizimba 18.
Bwana Mtei amesema malengo ya kampuni hiyo ni kuongeza vizimba vya kufugia samaki hadi kufikia vizimba 150, kujenga kiwanda cha chakula cha samaki na kupanua zaidi shughuli zake nyingine ili kuongeza tija zaidi katika biashara yake.
Bwana Mtei amesema katika awamu ya kwanza ya uvunaji wa samaki kampuni hiyo inatarajiwa kuvuna tani 50 za samaki na itachangia katika ukuaji wa pato la Taifa kwa kupitia kodi mbalimbali, mishahara na posho za watumishi na kuongeza mzunguko wa pesa katika jamii.
Tukio hilo limehudhuriwa na watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wakiongozwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Zabron Masatu, Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma na watumishi wa Manispaa hiyo na wafanyakazi na wadau wa Godwin Lusaso General Supply Co. Ltd.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa