Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini leo amezindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Mara amesema Serikali imeanza mchakato wa kuboresha usimamizi na usikilizaji wa mashauri yanayohusiana na ardhi.
“Mhe. Rais ameziagiza Wizara za Katiba na Sheria, Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mahakama kukutana ili kuhuisha mfumo wa usimamiaji wa mashauri ya ardhi hapa nchini” amesema Mhe. Sagini.
Mhe. Sagini amesema kwa sasa mfumo wa utoaji haki wa mahakama hapa nchini umeimarika sana na mashauri hayachukui muda mrefu sana kusikilizwa kama katika mabaraza ya ardhi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mabaraza katika baadhi ya maeneo ya utawala jambo ambalo linasababisha kero kwa wananchi.
Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Mara Mhe. Sagini amesema Serikali inaendelea na mchakato ili kuhakikisha mashauri hayo yanafanyika katika mfumo wa kawaida wa Mahakama ili kuboresha utoaji wa huduma za kisheria na utatuzi wa migogoro kwa wananchi.
Mhe. Sagini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Butiama akizungumzia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia amesema kampeni hiyo inalenga kuwapatia wananchi elimu juu ya upatikanaji wa huduma za kisheria bila malipo na kutoa mafunzo ya uraia na utawala bora kwa viongozi na watendaji katika nafasi mbalimbali.
Naibu Waziri huyo amesema tangu imeanza kufanyika hapa nchini, wananchi wengi wamejitokeza kuwasilisha malalamiko yao na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Marakujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo vizuri na hususan inapopita katika maeneo yao.
Mhe. Sagini amesema katika ushughulikiaji wa kesi za mirathi hamna ubaguzi wa wanawake na wanaume katika sheria na dhamira ya Serikali ni kujenga jamii yenye haki sawa kwa watu wote mbele ya sheria na vyombo vya kutoa maamuzi.
Akisoma salamu za Mkoa wa Mara, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Khalfan Haule ameiomba Serikali kufanya maboresho ya namna ya kushughulikia migogoro ya ardhi na hususan uundwaji wa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya.
Mhe. Haule ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rorya amesema baadhi ya Wilaya za Mkoa wa Mara hazina mabaraza jambo ambalo linalazimisha kutembea umbali mrefu kufuata huduma za mahakama hizo katika Wilaya nyingine.
Mhe. Haule ametoa mfano wa Wilaya za Butiama na Rorya ambazo hazina Mabaraza ya Ardhi na wananchi wake kulazimika kufuata huduma katika wilaya nyingine jambo ambalo linaleta usumbufu kwa wananchi.
Dkt. Haule amesema Mkoa una migogoro mingi ya ardhi na mabaraza ya ardhi yanachelewesha sana utatuzi wa migogoro jambo ambalo linaongeza kero kwa wananchi na kuiomba Serikali kufikiria namna ya kuzitumia mahakama za kawaida kushughulikia migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bwana Daudi James Mirumbe ameupongeza ushirikiano walioupata katika Mkoa wa Mara katika maandalizi ya uzinduzi wa Kampeni hiyo.
Bwana Mirumbe amewapongeza wadau wote waliosaidia kwa hali na mali kufanikisha uzinduzi wa kampeni hiyo katika Mkoa wa Mara kwa mafanikio makubwa na kuwaomba wananchi kutumia fursa hii ya siku tisa kutembelea mabanda ya maonyesho yatakayoendelea kuwepo katika viwanja hivyo.
Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia umefanyika katika Uwanjwa wa Mukendo, Manispaa ya Musoma ikiwa na kauli mbiu ya kampeni hiyo ni: Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa