Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 12 Desemba, 2024 amezindua Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa) na kuitaka Bodi hiyo kusimamia uboreshaji wa maboresho katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Mtambi amesema kuna nafasi ya kuweza kuziboresha huduma hizo baada ya uwekezaji mkubwa katika miundombinu, watumishi na vifaa tiba uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika hospitali hiyo.
“Bodi kama haitavaa viatu vyake, menejimenti ya Hospitali haitafanya kazi vizuri na wananchi hawatapata huduma zinazotegemewa na kupingana na adhma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi ameitaka Bodi hiyo kusimamia Sera, Sheria na miongozo ya Wizara ya Afya kuhusu utoaji wa huduma bure kwa wazee wasiojiweza, wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kupata huduma bure na kupunguza ukiritimba katika utoaji wa misamaha hiyo.
Mhe. Mtambi ameitaka bodi hiyo kutumia uzoefu wao, na taaluma zao katika kuisaidia na kuishauri Hospitali hiyokuwa wabunifu ili iweze kujiendesha na kuboresha huduma kwa wananchi na kupunguza rufaa kwenda katika hospitali nyingine za Rufaa.
Mhe. Mtambi ameitaka Menejimenti ya Hospitali hiyo kujipanga na kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusiana na huduma katika Hospitali hiyo na kumwagiza Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kuhakikisha kuwa huduma za vipimo inapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya muda wote bila kujali usiku, mwisho wa wiki na siku za sikuukuu.
Mhe. Mtambi amesema ofisi yake imejipanga kufuatilia utoaji wa huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki wakati wote kama inavyotarajiwa.
Mhe. Mtambi ametumia nafasi hiyo kuwataka watendaji wa Serikali wa Mkoa wa Mara kuhakikisha kuwa fedha zinazoletwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo inatumika vizuri
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wizara ya Afya Bi. Glory Laizer amesema Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere yenye wajumbe kumi imeteuliwa na Waziri wa Afya kwa mujibu wa Sheria tangu Januari, 2024 na itafanyakazi kwa miaka mitatu hadi 2027.
Bi. Laizer amesema mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa Bodi hiyo ulianzia Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mara ambaye mapendekezo ya wajumbe wa bodi hiyo ambayo ina mchanganyiko wa utaalamu na wanaotokana na wananchi wa Mkoa wa Mara na baadaye Waziri wa Afya aliwateua.
Bi. Laize amesema kwa sasa mafunzo ya wajumbe hao pamoja na menejimenti ya Hospitali hiyo yameanza jana ili kuwapitisha kuhusu majukumu na wajibu wa bodi na menejimenti katika utekelezaji wa mipango na uendeshaji wa Hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali hiyo Dkt. Hosea Bisanda amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watafanyakazi yao kwa ufanisi na watahakikisha katika muda wao wa uongozi wa miaka mitatu wataacha alama channya katika taasisi hiyo.
Dkt. Bisanda amesema kama Bodi hospitali hiyo itoe huduma nzuri na kupunguza rufaa za kwenda Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali za Taifa kulingana na wataalamu waliopo katika Hopsitali hiyo na kuifanya hospitali hiyo kuwa kimbilio la wananchi wanyonge.
Hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo zimehudhuliwa wajumbe wa Bodi hiyo, wawakilishi kutoka Wizara ya Afya, maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Menejimenti na baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa