Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo ameongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake kuhusiana na fursa tatu za nishati zinazotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) zenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na hususan wanaoishi katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza katika tukio hilo, Mhe. Mtambi amezitaja fursa zinazotolewa na REA kuwa ni pamoja na uuzaji wa majiko ya gesi yenye ruzuku, uuzaji wa mifumo ya umeme jua yenye ruzuku na mikopo ya riba nafuu ya kuanzisha vituo vya mafuta vijijini.
“Wananchi watumie nafasi hii iliyotolewa na Serikali kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hizi zinazotolewa na REA ili kuweza kubadilisha maisha yao ikiwa ni pamoja na kuanzisha biashara za kuuza mafuta katika maeneo ya vijijini” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema katika fursa ya uuzaji wa majiko ya gesi yaliyowekewa ruzuku, REA itayatoa majiko kwenye mitungu ya gesi ya kilo sita kwa gharama ya shilingi 20,000/= tu kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kuanzia mwezi januari, 2025.
Mhe. Mtambi amesema utoaji wa majiko hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mwezi Mei, 2024 na utekelezaji wa jukumu la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia hapa nchini ambalo wamepewa REA.
Mhe. Mtambi amesema fursa nyingine ni mikopo yenye riba nafuu ya kujenga vituo vya mafuta vijijini ambayo inatolewa kwa mtu mmoja mmoja au vikundi vya watu ambapo amewahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo yenye riba nafuu.
Kanali Mtambi amesema fursa nyingine ni uuzaji wa mifumo ya umeme jua mahususi kwa ajili ya wananchi wanaoishi maeneo ya visiwani na maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme kwa punguzo la asilimia hadi 75 ya bei za kawaida.
Mhe. Mtambi amesema fursa hizi zinatoa suluhisho la nishati safi ya kupikia, umeme wa gharama nafuu na mafuta na kuwahamasisha wananchi kuchangamkia fursa hizo zinazotolewa na Serikali.
Kwa Upande wake, Mhandisi Deusdedit Malulu kutoka Wakala wa Umeme Vijijini REA amesema wakala hiyo inatarajiwa kugawa mitungi ya kilo sita ya gesi pamoja na vifaa vyake 452,000 yenye thamani ya shilingi bilioni 8.6 hapa nchini.
“katika mitungi hiyo, Mkoa wa Mara utapewa mitungi ya gesi 19,350 yenye thamani ya shilingi milioni 350 ambapo kila wilaya inatarajiwa kupatiwa mitungi 3,255” amesema Mhandisi Malulu.
Mhandisi Malulu amesema wananchi watauziwa mitungi hiyo kwa gharama ya shilingi 20,000 na ili kuweza kununua mwananchi atatakiwa kuwa na namba au kitambulisho cha utaifa (NIDA) na kila mtu ataruhusiwa kununua jiko mmoja tu.
Mhandisi Malulu amesema REA inayo pia fursa ya wananchi kuuziwa mfumo wa umeme wa jua na vifaa vyake kwa punguzo la hadi asilimia 75 ya bei ya vifaa hivyo madukani ili kusogeza umeme wa uhakika na wa bei nafuu kwa wananchi wanaoishi mbali na umeme wa kawaida na hususan visiwani.
Mhandisi Malulu amesema REA pia inatoa mikopo ya hadi shilingi milioni 135 kwa mtu mmoja mmoja au vikundi kwa ajili ya uanzishwaji wa vituo vya mafuta vijijini kwa riba ya asilimia tano tu huku marejesho yanafanyika hadi miaka saba.
“Huu mkopo ni muafaka kwa watu wanaotaka kuanzisha biashara za mafuta katika maeneo ya vijijini na unalenga kupunguza ajali majumbani kwa wananchi wanaouza mafuta bila kufuata taratibu za uhifadhi wake” amesema Mhandisi Malulu.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Mhandisi wa TANESCO Mkoa wa Mara Mhandisi Nurdin Babu, baadhi ya maafisa kutoka REA makao makuu, maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya habari.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa