Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo ameongoza kikao cha Maafisa Elimu wa Halmashauri za Mkoa wa Mara na kuwataka Maafisa Elimu wa Halmashauri kusimamia kikamilifu suala la utoaji wa chakula shuleni kwa wanafunzi wa shule zote za kutwa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Bwana Kusaya amesema kwa sasa takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa asilimia 54.1 ya wanafunzi wote wa Mkoa wa Mara ndio wanapata chakula wakiwa shuleni jambo ambalo amesema halikubaliki.
“Fuatilieni michango ya wazazi na kama hawatoi kwa hiari zishaurini Halmashauri kutunga sheria ndogo ndogo ili kuwawezesha wazazi wa wanafunzi kuchangia kwa lazima na kuwawezesha wanafunzi wote wa kutwa kupata angalau mlo mmoja wakiwa shuleni” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amezipongeza Halmashauri ambazo angalau zimejitahidi na kuzitaka Halmashauri zote kutoa chakula kwa wanafunzi wote bila kufanya ubaguzi kwa wanafunzi kutokana na wazazi wao kutokuchangia chakula.
Bwana Kusaya amesema utoaji wa chakula shuleni ni maagizo ya Serikali na kama Mkoa hautasita kuwachukulia hatua maafisa watakaozembea au kukwamisha utekelezaji wa maagizo haya yanayolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
“Msitaka tuanze kufuatiliana kwenye utekelezaji wa jambo muhimu kama la utoaji wa chakula shuleni, timizeni wajibu wenu na mhakikishe watoto wote wanakula wawapo shuleni” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amesema utoaji wa chakula ni suala muhimu sana katika maendeleo ya elimu ya Tanzania na nchi isipokuwa na wananchi walioelimika inakuwa vigumu kwa nchi hiyo kupata maendeleo endelevu.
Aidha, amewataka Maafisa Elimu kuwashirikisha viongozi wa Halmashauri zao na ofisi za Wakuu wa Wilaya katika uhamasishaji wa wazazi na walezi kuchangia chakula shuleni na kama kuna changamoto Mkoa pia utaarifiwe kuhusiana na changamoto za utekelezaji wa maagizo hayo ili uweze kuchukua hatua stahiki mapema.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga amesema kikao hicho cha Maafisa Elimu wa Halmashauri kinafanyika kila baada ya miezi miwili kikiwa na lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali.
Bwana Bulenga amesema katika kikao hicho kwa kuwa ni mwisho wa mwaka watafanya tathmini ya mambo yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka mzima na kuweka mipango na mikakati ya utekelezaji wa shughuli kwa mwaka 2025.
Bwana Bulenga ametumia fursa hiyo kumuomba Katibu Tawala wa Mkoa kuangalia upya maombi ya uhamisho wa walimu kwa kuwa walimu wengi wanaomba kuhama kuliko wanaokuja katika Mkoa wa Mara.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Maafisa Elimu wote wa Halmashauri, Wadhibiti Ubora na baadhi ya Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na kimefanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa