Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo ameongoza kikao cha Maafisa Elimu wa Halmashauri za Mkoa wa Mara na kuwataka maafisa elimu hao kuhakikisha wanapandisha ufaulu katika matokeo ya Darasa la Saba na Kidato cha Nne.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Bwana Kusaya amesema kwa sasa ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi umepanda kutoka asilimia 74 mwaka 2022 hadi asilimia 78 mwaka 2024 lakini hata hivyo anahitaji ufaulu zaidi.
“Tunatakiwa kufanya vizuri ili Mikoa mingine walete wataalamu wao kuja kujifunza Mkoa wa Mara namna ya kusimamia ujifunzaji na ufundishaji na kupata matokeo mazuri, ninajua hili tukiongeza juhudi linawezekana” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amezipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa kupandisha asilimia za ufaulu kila mwaka kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2022 hadi 2024.
Aidha, Bwana Kusaya amezipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kwa kuongoza katika matokeo ya Darasa la Saba mwaka 2024 na kuzikemea Halmashauri za Manispaa ya Musoma, Halmashauri ya Mji wa Bunda na Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kufanya vibaya katika matokeo hayo.
“Ninyi mliopo mjini nilitegemea mfanye vizuri zaidi kuliko Halmashauri za Wilaya lakini hamfanyi vizuri ukilinganisha na Halmashauri za Wilaya ambazo zina mazingira mabaya na zina shule nyingi zaidi lakini zinafanya vizuri” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amewataka Maafisa Elimu hao kusimamia ujifunzaji na ufundishaji na kuhakikisha walimu wote wanaingia madarasani kufundisha na kuhakikisha walimu wote ambao hawana likizo au ruhusa wanakuwepo shuleni hata kama hawana vipindi kwa siku husika.
Aidha, amewataka kufanya ufuatiliaji wa watoto wanaotakiwa kuandikishwa darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza na kuhakikisha wakati huu wa likizo walimu wanakuwepo shuleni ili kuwapokea wazazi wanaokuja kuwaandikisha wanafunzi.
“Ni marufuku kuruhusu michango wakati wa uandikishaji wa wanafunzi” amesema Bwana Kusaya na kuwataka Maafisa Elimu hao kufuatilia suala hilo ili kuwezesha watoto wengi zaidi na hususan wenye mahitaji maalum kuweza kuandikishwa shuleni.
Aidha, amewataka Maafisa Elimu kufuatilia miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuboresha mazingira ya ufundishaji, ujifunzaji na nyumba za watumishi katika maeneo yao na kuwataka kuacha kukaa maofisini.
Bwana Kusaya amewataka Maafisa Elimu kuweka mipango ya kuboresha asilimia ya wanafunzi wanaomudu kusoma, kuandika na kuhesabu ambapo amesema kwa sasa Mkoa una wastani wa asilimia 80 na kuwataka kuongeza juhudi ili ifikie asilimia 100.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa kwa kuweza kufungua kikao hicho na kumuahidi maagizo yote aliyoyatoa Idara yake itasimamia utekelezaji wake.
Bwana Bulenga amemuahidi Katibu Tawala kusimamia ufundishaji na ujifunzaji ili kuleta mabadiliko zaidi katika ufaulu wa wanafunzi wa madarasa yote na kuboresha asilimia ya wanafunzi wanaoweza kumudu kusoma, kuandika na kuhesabu katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Bwana Bulenga amesema atasimamia mafunzo kwa walimu wa masomo ambayo hayafanyi vizuri ili kuwajengea uwezo kutumia fedha zilizopangwa katika Mradi wa Shule Bora unaotekelezwa katika Mkoa wa Mara ambazo tayari zimepokelewa katika Halmashauri zote.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Maafisa Elimu wote wa Halmashauri, Wadhibiti Ubora na baadhi ya Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na kimefanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa