Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo amezindua rasmi Tawi la Benki ya CRDB katika eneo la Mugango na kuwataka wananchi wa Wilaya ya Musoma kutumia huduma za benki katika kutunza fedha na kuendesha biashara zao.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa tawi hilo, Bwana Kusaya amesema kuna faida nyingi kwa wananchi kutunza fedha zao benki ikiwa ni pamoja na usalama wa fedha dhidi ya majanga, wizi, urahisi wa kupata mikopo ya biashara na urahisi wa kufanya malipo kutumia mifumo ya kidijiti ya benki.
“Mtu akitumia benki itakuwa ni rahisi kwa benki inayotaka kumpatia mkopo wa biashara kufuatilia rekodi za mapato na matumizi katika biashara hiyo ili kumwezesha kupata mkopo kama atahitaji” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya ameipongeza Benki ya CRDB kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Sekta ya Fedha hapa nchini na kuitaka benki hiyo kutoa mikopo yenye masharti na riba nafuu kwa wananchi ili kuwahamasisha kuachana na mikopo inayotolewa na wafanyabiashara wanaotoza riba kubwa.
Aidha, Bwana Kusaya ameitaka Benki ya CRDB kuendelea kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa umma na kuwahamasisha wananchi kutumia benki katika kuhifadhi fedha zao na kuendesha na kusimamia biashara zao.
Bwana Kusaya amewataka wananchi watakaopata mikopo ya biashara katika benki hiyo kurejesha mikopo mapema ili kuwajengea uaminifu katika Benki hiyo na benki nyingine na kuwawezesha kupata mikopo wakati mwingine ya kuendeleza biashara zao.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Bwana Boma Raballa amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara na wageni wote walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Tawi la Mugango kwa kuweza kushiriki.
Bwana Raballa amesema kuwa Benki hiyo inayo matawi zaidi ya 250 na machine za kutolea fedha zaidi ya 550 pamoja na mawakala waliosambaa na kutoa huduma katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Bwana Raballa amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa jitihada zake za ufuatiliaji na kuhakikisha Benki ya CRDB inafungua tawi katika eneo la Mugango akiamini wananchi wake hawawezi kuendelea bila ya kupata benki ya uhakika katika eneo hilo.
Bwana Raballa amewataka wakulima, wavuvi na wafugaji kuchangamkia akaunti mpya za kilimo za Benki ya CRDB ambazo hazina makato na kwa baadae zitawasaidia katika kupata mikopo inayotolewa na benki hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa Bwana Lusingi Sitta amesema kuwa kwa sasa baada ya kufungua Tawi la Mugango, Benki ya CRDB ina matawi tisa katika Mkoa wa Mara na tawi jingine la kumi linatarajiwa kufunguliwa katika Mkoa wa Mara karibuni.
Bwana Sitta amesema Tawi la Mugango linatarajiwa kutoa huduma zote za kibenki ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti, kutoa mikopo, kutoa ushauri wa kibiashara kwa wafanyabiashara wadogo na kuwahudumia wateja wakubwa na wadogo wa benki hiyo.
Bwana Sitta amewapongeza wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa mwitikio mkubwa katika kuitumia benki hiyo na hususan wakulima, wavuvi na wafanyabiashara za samaki waliopo katika eneo hilo.
“Tangu Tawi la Mugango lilipoanza kufanyakazi Aprili, 2024 mpaka sasa tayari tumepata wateja zaidi ya 1000 waliofungua akaunti mpya za benki na wanaopata huduma katika tawi hili” amesema Bwana Sitta.
Bwana Sitta amewataka watumishi wa taasisi mbalimbali zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kuitumia benki hiyo badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibenki katika Manispaa ya Musoma.
Tawi la Mugango la Benki ya CRDB limeanza kutoa huduma kwa wananchi kuanzia mwezi Aprili, 2024 na linatoa huduma kwa taasisi mbalimbali za Serikali, binafsi na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa