Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amezungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake na amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Mara usalama katika kipindi chote cha sikukuu za Noeli na Mwaka Mpya.
“Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa Mkoa wetu unakuwa eneo salama wakati wote wa sikukuu hizi za mwisho wa mwaka” amesema Mhe. Mtambi,
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kutii sheria bila shuruti na kujiepusha na vitendo vya kiuhalifu na ametoa onyo kwa wanaopanga kufanya uhalifu wakati huu wa sikukuu kuacha kwani vyombo vya usalama vimejipanga kukabiliana na vitendo vya kihalifu.
Mhe. Mtambi amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza doria katika maeneo yote wanayoishi wananchi na kuchukua hatua stahiki za kuzuia ajali barabarani kwa kuwadhibiti madereva wanaoendesha vyombo vya moto kwa uzembe na kuhatarisha maisha ya watu na mali zao.
“Ninawataka Askari wa Usalama barabarani kuanzia leo kuwa wakali kweli kweli na kuwachukulia hatua za kisheria madereva wazembe barabarani,….hatuko tayari kuona wananchi wakipata madhira kipindi hiki cha sikuukuu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi kutokuendesha vyombo vya moto wanapokuwa wamekunywa vileo na kuwataka kuchukua tahadhari za usalama ili kulinda usalama wao na familia zao wakati huu wa sikukuu.
Mhe. Mtambi amewataka wazazi na walezi kuendelea kusimamia maadili ya watoto wadogo kwa kuwazuia kwenda kwenye kumbi za starehe bila ya kuwa na uangalizi wa kutosha na hususan nyakati za usiku.
Kanali Mtambi amewakumbusha wazazi na walezi wakati wanasherekea sikukuu kukumbuka kutenga fedha za ada na mahitaji muhimu ya shule kwa ajili ya watoto ili kuwawezesha watoto kwenda shule shule zitakapofungua tena.
Mhe. Mtambi ametumia pia fursa hiyo kuwatakia wananchi wote wa Mkoa wa Mara heri ya sikukuu ya Noeli na Mwaka Mpya, 2025.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa