Mkoa wa Mara umewataka wajasiriamali wanawake kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa makundi ya vijana, watu wenye ulemavu na wanawake ili kukuza na mitaji na kupanua biashara zao.
Hayo yameelezwa katika hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi iliyosomwa na Dkt. Omari Gamuya leo tarehe 12 Machi, 2025 alipomwakilisha katika kufunga kongamano la wajasiriamali lililoandaliwa na Shirika la Powerlife lililofanyika katika ukumbi wa uwekezaji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara zimetoa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri yenye jumla ya shilingi 2,472,345,193.17 kwa makundi hayo.
“Ninawataka wajasiriamali wanawake kuchangamkia fursa za mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri ili kuongeza mitaji na kuboresha biashara zenu na maisha yenu kwa ujumla” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wajasiriamali hao kuchangamkia fursa za kibiashara katika nchi jirani baada ya Serikali ya awamu ya sita kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kufanyabiashara zao bila wasiwasi katika nchi hizo.
Aidha, amelipongeza Shirika la Powerlife kwa kuandaa kongamano hilo na kufanya maonyesho katika Wilaya ya Serengeti na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia elimu na ujuzi watakaoupata kuboresha biashara zao na maisha yao.
Mhe. Mtambi amesema Mkoa wa Mara unazo fursa nyingi katika sekta mbalimbali na unaunga mkono shughuli za shirika hilo kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika Mkoa na maeneo mengine nje ya Mkoa.
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kuwataka wajasiriamali hao kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuunga mkono kampeni ya matumizi ya nishati bora inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Biashara na Viwanda Bwana Gambaless Timotheo amewataka wajasiriamali hao kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo vidogo (SIDO) kuchangamkia fursa za ongezeko la mahitaji ya dagaa waliosindikwa ambao hawana mchanga.
“Chachu ya mafunzo haya ya leo inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa washiriki na jamii kwa ujumla kama yatachukuliwa kwa uzito unaostahili kwa washsiriki wote waliopo hapa” amesema Bwana Timotheo.
Bwana Timotheo amesema SIDO imeanza kutoa mafunzo kwa wajasiriamali kuhusiana na fursa ya soko la dagaa waliosondikwa na kuwawezesha wajasiriamali utaalamu wa kusindika dagaa na kuwataka wajasiriamali hao kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali ikiwemo Halmashauri.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi na mwanzilishi wa Shirika la Powerlife Bi. Mariam Suleiman amesema kongamano hilo limehudhuriwa na wajasiriamali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Halmashauri ya Mji wa Bunda, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Halmashauri ya Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
“Kongamano linguine kama hili tumelifanya katika Wilaya ya Tarime jana lililohusisha Halmashauri za Tarime Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya” amesema Bi Mariam Suleiman.
Amesema katika makongamano hayo, shirika hilo limekuwa likishirikiana na Halmashauri, SIDO, Mamlaka ya Mapato (TRA), NSSF na wadau wengine kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake wajasiriamali wa Mkoa wa Mara.
Bi. Mariam Suleiman amesema kuanzia tarehe 01 hadi 07 Machi, 2025 shirika hilo limefanya maonesho ya shughuli mbalimbali katika Wilaya ya Serengati likiwa na lengo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kujikwamua kiuchumi kupitia fursa mbalimbali za maendeleo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa