Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo amezungumza na Waandishi wa Habari kuhusu uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Mara utakaofanyika tarehe 11 Desemba, 2024 katika Uwanja wa Mukendo, Manispaa ya Musoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake, Bwana Kusaya amewataka wananchi kushiriki uzinduzi wa kampeni hiyo na katika Kata, Mitaa na Vijji vitakavyofikiwa na kampeni hiyo katika Mkoa wa Mara.
“Hii ni fursa kubwa ambayo Serikali imeileta kwa wananchi kuweza kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria, uraia na utawala bora na huduma zote zitatolewa bure bila malipo yoyote” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amesema Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Kampeni hiyo katika Mkoa wa Mara atakuwa ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (MB.) na kauli mbiu ya kampeni hii ni “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo”.
Bwana Kusaya amesema kwa wakati huu, kampeni hii inaendeshwa katika mikoa minne hapa nchini ambayo ni Iringa, Songwe, Mara na Morogoro.
Bwana Kusaya amesema kampeni hii itatekelezwa katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara na kuzifikia Kata 10 kwa kila Halmashauri na Mitaa/Vijiji vitatu kwa kila Kata katika kipindi cha siku tisa kuanzia tarehe 11 Desemba, 2024 hadi tarehe 20 Desemba, 2024.
Wakati huo huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya amefungua kikao kazi cha wataalamu kuhusiana na uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria kinachoendelea katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kuwataka wataalamu wanaoshiriki kikao hicho kutoa ushirikiano.
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Bwana Kusaya amewataka wataalamu walioshiriki kikao hicho kusikiliza kwa makini na kutoa ushirikiano kwa waandaaji ili kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Mara Bwana Laurent Burilo amesema katika kampeni hii, wanatarajia kuzifikia Halmashauri zote na Kata 10 na vijiji/ mitaa mitatu katika kila kata.
Bwana Burilo amesema mpaka sasa katika mikoa iliyopita wamehudumia wananchi wengi na changamoto kubwa walizoziona ilikuwa ni uelewa wa masuala ya sheria, migogoro ya ardhi na ukatili wa kijinsia.
“Katika mikoa ambayo tayari imefikiwa na kampeni hii kuna maeneo mengi wanaume wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia walijitokeza na kuwasilisha malalamiko yao kwa wataalamu na wakapatiwa msaada wa kisheria” amesema Bwana Burilo.
Bwana Burilo amesema katika kampeni hii pia elimu kuhusu masuala ya Uraia na Utawala Bora itatolewa kwa kushirikiana na wadau.
Bwana Kusaya amesema kampeni hii ilianza kutekelezwa Mkoa wa Dodoma tarehe 28 Mei, 2023 baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) tarehe 27 Mei, 2023 Jijini Dodoma na mpaka sasa Kampeni hii imeshafanyika katika mikoa mingine saba.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inafanyika hapa nchini kwa miaka mitatu kuanzia mwezi Machi, 2023 hadi mwezi Februari, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa