Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Majaliwa Kassim (MB), leo tarehe 25 Machi, 2025 kupitia simu ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, amezungumza na wananchi waliopata maafa katika Manispaa ya Musoma.
Akizungumza katika tukio hilo, Mhe. Majaliwa ametoa pole sana kwa wananchi wa Manispaa ya Musoma walioathirika na tukio hilo na kuongeza kuwa wataalamu wa maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wapo njiani kwenda Musoma kuungana na timu za maafa za Wilaya na Mkoa kwa ajili ya kushughulikia maafa hayo.
“Tumeshamleta mtaalamu wa Maafa ameondoka alfajiri leo Dodoma anakuja kuungana na timu ya maafa hapo Musoma na atakapofika watashirikiana kufanya uratibu wa masuala hayo ili Serikali ione namna nzuri ya kusaidia kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwenye eneo hilo” amesema Mhe. Majaliwa.
Mhe. Majaliwa amesema, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezungumza naye na kutoa salamu za pole za Mhe. Rais kwa wananchi wa Manispaa ya Musoma walioathirika katika maafa hayo.
Mhe. Majaliwa amewataka wananchi kuwa watulivu lakini pia watoe ushirikiano kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya ili waweze kushughulikia vizuri jambo hilo na hatimaye Serikali iweze kujua namna nzuri ya kuwasaidia.
Baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Mtambi ametoa pole kwa wananchi wote walioathirika na kuwahakikishia kuwa Serikali inafanya tathmini na inajipanga kuhusu namna bora ya kuwasaidia.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka wananchi kuwa na uvumilivu wakati huu Serikali inaporejesha huduma muhimu za kijamii katika maeneo hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa