Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amefungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo viongozi wa kamati za maendeleo (CDC) wa Kata na Vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na kuwataka viongozi kusikiliza na kushughulikia utatuzi wa kero za wananchi.
“Jukumu kubwa la kiongozi ambalo ninawatakeni mkalitekeleze ni kutatua kero na changamoto za wananchi, hilo ninaomba mkalitekeleze. Mhakikishe mnawasikiliza wananchi na mshirikiane nao kutafuta suluhu ya hizo changamoto” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka viongozi hao kuwasilisha ngazi inayofuata changamoto ambazo wanaona hawawezi kuzitatua wenyewe na kufuatilia kuhakikisha ufumbuzi wa changamoto hizo unapatikana ili kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka viongozi walioshiriki mafunzo hayo kwa kupitia Kamati za Maendeleo (CDC) kuibua miradi yenye manufaa kwa jamii itakayoweza kuibadilisha huduma za kijamii na uchumi wa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Mhe. Mtambi ameupongeza Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo amsesema ni muhimu kwa viongozi hao kupata mafunzo hayo ya uongozi na hususan baada ya kuchaguliwa kuongoza vijiji na vitongoji ambapo itawapasa kuzingatia miiko na misingi ya uongozi ikiwa ni pamoja na utawala bora na kutenda haki kwa wanaowaongoza.
“Wengi wetu tunafikiri kuwa uongozi ni kuamua tu, uongozi hauko hivyo………..inakupaswa kuzingatia miiko na misingi ya uongozi…….ili jamii inapokabiliwa na changamoto yoyote ile upate nafasi ya kutoa ushauri au dira ya nini hasa kifanyike kutatua changamoto inayoikabili jamii” amesema Mhe. Mtambi.
Amewapongeza wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwa ushindi walioupata katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kusema kuwataka kuwaonyesha dira ili kuwapeleka wananchi kwenye maendeleo.
Mhe. Mtambi amewataka viongozi hao kuvikataa vitendo na tamaduni zilizozoeleka katika jamii ambavyo havileti picha nzuri katika jamii ili kuwahakikishia wananchi na watalii usalama na amani katika maeneo ya Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amesema Mkoa wa Mara unaovivutio vingi ambavyo vinaweza kuwavutia watalii lakini wananchi na viongozi wasipokemea vitendo vya vibaya inaweza kukwamisha jitihada mbalimbali za Serikali za kujenga miundombinu ya utalii.
“Pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ili kuwavutia watalii, kama jamii haitabadilika na kulinda amani na usalama bado watalii hawataweza kuja kwa wingi Mara kama ilivyo katika mikoa mingine” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wakazi wa eneo la Nyabirama 171 ambao bado hawajachukua fidia zao kujitokeza na wengine 11 ambao wamegoma kufidiwa na kupisha uwekezaji wa mgodi katika eneo hilo waendelee kuelimishwa kuhusu umiliki wa ardhi na athari za wao kuendelea kuwa maeneo hayo wakati shughuli za mgodi zikiendelea.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara Bwana Apolinary Lyambiko amesema mafunzo hayo ya siku tatu yanatolewa kwa viongozi wa jamii kutoka Kata na Vijiji vinavyozunguka mgodi.
Bwana Lyambiko amesema kwa kutambua umuhimu wa kujielimisha na kuna viongozi wapya katika maeneo hayo waliona kuna haja ya kuwajengea uwezo na kuleta uelewa wa pamoja juu ya masuala ya utawala bora, usimamizi wa Sheria na masuala ya ardhi.
Bwana Lyambiko amewataka viongozi waliohudhuria mafunzo hayo kutumia fursa ya mafunzo hayo kuboresha utendaji wao katika maeneo yao ya kazi pamoja na kuboresha utatuzi wa migogoro ya wananchi katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mhe. Mwita Waitara amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka baada ya viongozi wapya wa vijiji kuingia madarakani katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchini Novemba 27, 2024 ili waende kusimamia miradi ya maendeleo katika vijiji hivyo.
Mhe. Waitara amesema vijiji hivyo vinapata fedha nyingi kutokana na ujirani wao na mgodi huo ikiwemo fedha za asilimia moja, mrabaha na makusanyo mengine ya Halmashauri hivyo fedha hizo zikitumika vizuri kutekeleza miradi ya maendeleo zitabadilisha maisha ya wananchi.
Mhe. Mwita amesema kwa mwaka huu vijiji hivyo vimepokea fedha za asilimia moja jumla ya bilioni 6.1 kwa vijiji vyote 11 vinavyozunguka mgodi na kuwa fedha hizo zikitumika vizuri kwa kutoa vipaumbele kwenye miradi inayoinua maisha ya wananchi, hali ya wananchi inaweza kubadilika.
Aidha, Mhe. Waitara amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Mara kufuatilia matumizi ya fedha za Mfuko wa Hisani unaotumika kusomesha wanafunzi kutoka kaya maskini ambao ametilia mashaka matumizi ya fedha za mfuko huo.
Mhe. Waitara pia ameushauri Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kuacha kusambaza taarifa za maeneo wanayotarajia kuyachukua kutoka kwa wananchi ili kupunguza tegesha na migogoro ya ardhi na wananchi wanaouzunguka mgodi huo.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, baadhi ya Madiwani na watendaji wa wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji, wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC), viongozi wa dini wa vijiji kumi vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa