Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Afred Mtambi leo ameongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ngazi ya Mkoa kwa kipindi cha Julai- Desemba kwa mwaka 2024/2025 na kuzitaka Halmashauri kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe.
“Halmashauri zitoe kipaumbele katika utekelezaji wa mkataba wa lishe katika vipengele vyote ili kuufanya Mkoa kushika nafasi nzuri katika tathmini ya utekelezaji wa mkataba huo kitaifa” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewapongeza viongozi na wataalamu kwa namna mlivyotekeleza na kusimamia mkataba huu kwa mwaka 2023/2024 ambapo Halmashauri zilitenga fedha na kufanya matumizi kwa masuala mbalimbali ya lishe kwa asilimia 95 na kuzitaka Halmashauri kuendelea kuboresha.
Mhe. Mtambi amezipongeza Halmashauri kwa kuendelea kuboresha utengaji na matumizi ya fedha kwa ajili ya afua za lishe na kuzitaka Halmashauri zinapotengeneza makisio ya bajeti yam waka wa fedha 2025/2026 kutumia bajeti ya mwaka 2024/2025 au kufanya maboresho katika utengaji wa fedha za afua za lishe.
Kanali Mtambi amewaonya wataalamu na hususan Wahasibu na Maafisa Manunuzi wa Halmashauri kwa kuchelewesha utoaji wa fedha na manunuzi yanayohusiana na masuala ya lishe na kuwataka kutoa kipaumbele katika masuala ya lishe.
Aidha, amemtaka Afisa Lishe Mkoa wa Mara kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa mkataba wa lishe kila mwezi ili aweze kujua maendeleo ya utekelezaji wa mkataba huo kwa Halmashauri mbalimbali na kuchukua hatua stahiki kabla ya kikao cha tathmini ya Kitaifa kitakachofanyika baadaye mwaka huu.
Mhe. Mtambi amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha matumizi yote ya fedha za lishe katika Halmashauri za Mkoa wa Mara yanaingizwa katika Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE) na kuhakikisha Halmashauri zinafanya siku ya lishe ya kijiji au mtaa kulingana na miongozo ya masuala ya lishe.
Mhe. Mtambi amempongeza Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Bwana Bundi Clement Chaula ambaye pamoja na kuwa yupo Afisa Lishe mmoja katika Halmashauri hiyo amekuwa mfano mzuri kitaifa wa utoaji wa taarifa za lishe na tayari Halmashauri nyingine zinakuja kujifunza Musoma DC.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Mkoa wa Mara Bibi Grace Martin amesema Mkoa wa Mara umepanga kupunguza changamoto ya udumumavu, uzito pungufu kwa watoto na watu wazima, kuongeza vifaa vya utambuzi, kuongeza vituo vya matibabu ya utapiamlo, kuongeza uhamasishaji wa jamii kuhusiana na lishe.
Bibi Martin amesema katika matumizi ya fedha kwa Halmashauri kati ya Julai- Desemba, 2024 Halmashauri sita kati ya tisa zimepata alama za njano na nyekundu na hivyo Mkoa una wastani wa asilimia 50.01 na kuzitaka Halmashauri husika kuongeza matumizi ya fedha.
Bibi Martin ameyataja mafanikio wanayopata kuwa ni pamoja na kuwa na maafisa lishe zaidi ya mmoja katika HAlmashauri nane kati ya tisa; Halmashauri za Mkoa wa Mara kuanza kutenga bajeti kwa ajili ya utafiti wa masuala ya lishe katika maeneo yao, na siku ya lishe ya mfano Kitaifa kwa mwaka 2024 ilifanyika Musoma DC kutokana na utendaji kazi wa Afisa Lishe wa Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Omari Gamuya amesema Kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ngazi ya Mkoa ni mwendelezo wa vikao vinavyoanzia kwenye ngazi ya kata na baadaye katika Halmashauri kwa kila robo mwaka.
Dkt. Gamuya amesema kwa ngazi ya Mkoa, vikao hivi vinafanyika mara mbili kwa mwaka na Mkoa unatakiwa kuwasilisha taarifa katika kikao cha Tathmini ya Kitaifa ambacho kinafanyika kwa mwaka mara moja.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa