Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza mafunzo kuhusu Uraia na Utawala Bora kwa Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Musoma na Menejimenti ya Sektretarieti ya Mkoa wa Mara na kuwataka washiriki kushiriki kikamilifu mafunzo hayo na kutumia elimu watakayopata kuboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Mtambi amewataka viongozi walioshiriki mafunzo hayo kufuatilia mafunzo hayo na kuuliza maswali kwa wataalamu hao ili kuboresha utoaji wa huduma na utatuzi wa kero za wananchi wa Mkoa wa Mara.
“Mafunzo ni muhimu sana katika utekelezaji wa majukumu yetu na yanatukumbusha namna ya kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu tunapotoa huduma kwa wananchi na kutatua kero zinazowakabili wananchi” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kuwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwatendea haki wananchi kwa kutimiza wajibu wao kikamilifu na kuwasaidia kutatua kero zinazowakabili katika maeneo yao.
Mhe. Mtambi amezishukuru Wizara za Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kuwezesha mafunzo hayo muhimu kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa Mkoa wa Mara ambayo yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuandaa, kuratibu na kuendesha mafunzo hayo kwa Kamati za Usalama za Mkoa, Wilaya, viongozi na Watendaji wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Bwana Kusaya amesema mafunzo hayo yatawasaidia watumishi kuboresha huduma na utatuzi wa kero na changamoto za wananchi na kuiomba Wizara ya Katiba na Sheria kutoa mafunzo hayo mara kwa mara kwa makundi mbalimbali ili kuyafanya mafunzo hayo kuongeza tija.
“Mafunzo ya aina hii yanapaswa kuletwa mara kwa mara ili viongozi na watendaji wengi zaidi waweze kufikiwa na kupatiwa mafunzo haya ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi” amesema Bwana Kusaya.
Akitoa mada katika mafunzo hayo, Bwana Nicolaus Mhagama kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia elimu waliyoipata katika mafunzo hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu mambo mbalimbali ya kitaifa yanayofanywa na Serikali.
Bwana Mhagama amewataka viongozi hao kuwaelimisha wananchi kuhusu taratibu za kisheria, kanuni na taratibu za kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili na hususan namna ya kufanya mashauri yanapokuwa yamefikishwa mahakamani.
Bwana Mhagama amewataka viongozi kusimamia uadilifu wa watendaji waliopo chini yao na hususan katika ngazi za Kata, Mitaa, Vijiji na Vitongoji ambao wanawahudumia wananchi katika utendaji wao wa kila siku ili kuwafanya wananchi kuongeza imani kwa Serikali yao.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji ni sehemu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia iliyozinduliwa tarehe 11 Desemba, 2024 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini katika Uwanja wa Mukendo, Manispaa ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa