Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 27 Machi, 2025 ameandaa futari kwa ajili ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwataka viongozi wa dini kuisaidia Serikali katika kulinda maadili katika jamii na amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza na washiriki wa futari hiyo iliyofanyika nyumbani kwake katika Mtaa wa Mukendo, Manispaa ya Musoma, Mhe. Mtambi amewataka viongozi wa dini kukemea mmomonyoko wa maadili katika jamii ili kuijenga jamii yenye maadili mema.
“Tuwakumbushe waumini wetu kuhusu kufuatilia maadili ya watoto katika jamii yetu ili kujenga kizazi chenye maadili mema na kuwafanya watu kuwa na hofu ya Mungu katika maisha yao” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka viongozi wa dini kukemea malezi yanayofanywa na mitandao ya kijamii na badala yake amewataka viongozi hao kuwahamasisha waumini wao katika kuwajibika katika malezi kama wazazi na walezi wa watoto na sio kuiachia mitandao ya kijamii.
Mhe. Mtambi amewataka viongozi wa dini kuhamasisha amani na utulivu uliopo katika nchi yetu uendelee hata wakati wa uchaguzi mkuu ili uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu na usiwe kama njia ya kuhalalisha uhalifu kwa watu wanaopenda kufanya hivyo.
Kanali Mtambi amewataka viongozi wa dini kukemea vitendo vyovyote vya kuvuruga amani wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi na kuwataka kuombea amani, umoja na ushirikiano kwa wananchi wote ili nchi yetu ijikite zaidi katika kutekeleza shughuli za maendeleo na sio mapigano.
Mhe. Mtambi amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwaombea viongozi na amani ya nchi ya Tanzania ili iendelee kuwepo na kuuombea Mkoa uweze kuepukana na majanga mbalimbali na uweze kufanya vizuri katika shughuli za maendeleo.
Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi wa dini kuwahamasisha wazazi kuhusu elimu ya watoto wao na kutoa mfano mwaka 2025 wanafunzi wa kidato cha kwanza wengi hawakuanza shule hadi Serikali ya Mkoa ilipowafuatilia wazazi na walezi wa wanafunzi hao.
“Pamoja na uwekezaji wa Serikali katika elimu, bado wazazi wengi hawana mwamko wa kuwapeleka watoto wao shule jambo ambalo linaufanya uwekezaji huu uwe ni kazi bure, sisi kama Serikali hatutakubali” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kutokumpeleka mtoto shule, kutochangia chakula ili mtoto ale akiwa shuleni ni ukatili kwa watoto kwa sababu unawanyima watoto haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka viongozi wa dini kukemea mila za ukeketaji, jamii kujichukulia sheria mkononi, ubabe usio na msingi na kusema kuwa kwa Mkoa wa Mara mambo kama hayo yamepitwa na wakati na badala yake viongozi wa dini wahamasishe waumini kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kuuinua Mkoa wa Mara kiuchumi.
Futari hiyo pamoja na viongozi wa dini ilihudhuriwa pia na Kamati ya Usalama ya Mkoa, viongozi wa ngazi mbalimbali, taasisi za umma na taasisi binafsi na wawakilishi wa waumini wa dini na madhehebu mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa