Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ametoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu kambi ya madaktari bingwa 40 watakaotoa huduma Hopitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Kwangwa kuanzia tarehe 2-6 Desemba, 2024 na kuwataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa madaktari hao kutibiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mhe. Mtambi amesema madaktari bingwa hao wanatoka katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Hospitali za Rufaa za Kanda za Bugando na Chato ambao watatoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.
“Hii ni fursa adhimu ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeisogeza kwa wananchi wa Mkoa wa Mara wakiitumia itawapunguzia adha ya kusafiri kufuata huduma” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema huduma za madaktari hao zitakuwa na faida zaidi kwa mgonjwa kwani katika siku hizo mgonjwa anaweza kuonwa na madaktari bingwa zaidi ya mmoja ambao wanaweza kubadilishana uzoefu tofauti na akienda katika matibabu ya kawaida kama atafanikiwa kumpata daktari bingwa atakuwa mmoja.
Mhe. Mtambi amesema maganjwa yatakayotibiwa katika kambi hiyo pamoja na magonjwa ya akina mama na uzazi, magonjwa ya pua, koo na masikio, afya ya akili, magonjwa ya ndani yanayojumuisha magonjwa ya kisukari, presha, figo na kadhalika na magonjwa ya kinywa na meno.
Aidha, madaktari hao watatoa huduma za kibingwa za radiolojia, dawa za usingizi na kufanya upasuaji wa kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu amesema kambi ya madaktari bingwa hao inategemewa kufanyika katika muda wa kazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni.
Dkt. Masatu amesema malengo ya Serikali kuleta madaktari bingwa hao ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, kuwajengea uwezo wataalamu wa afya waliopo katika utoaji huduma za kibingwa na kuibua wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa watakaotibiwa katika Hospitali za Rufaa za Kanda.
Dkt. Masatu amesema madaktari bingwa hao wanatoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Kegera, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga na hospitali za Rufaa za Kanda za Chato iliyopo Mkoa wa Geita na Bugando iliyopo Mkoa wa Mwanza.
Hii ni mara ya tatu mwaka huu Serikali inaleta madaktari bingwa katika Mkoa wa Mara kwa ajili ya matatibabu ya kibingwa hata hivyo awali madaktari bingwa hao walikuwa wanaletwa katika Hospitali za Halmashauri za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa