Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 05 Machi, 2025 ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji na kuwataka wakurugenzi kuweka mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.
Mhe. Mtambi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa kukusanya asilimia 78 hadi Desemba, 2024 huku Halmashauri ya Mji wa Tarime ikikusanya asilimia 32 tu ya makadirio ya mapato ya ndani hadi kufikia Desemba, 2024.
Mhe. Mtambi amezitaka Halmashauri ambazo hazikufanya vizuri ziongeze juhudi katika makusayo ili kuweza kuimarisha huduma za jamii katika maeneo yao.
Mhe. Mtambi pia amezitaka Halmashauri kuendelea kuweka kuchangia asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amemtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (MUSOMA) kukutana na viongozi wa Wilaya ya Tarime na Halmashauri ya Mji wa Tarime kujadili mkakati wa muda mfupi kutatua tatizo la upatikanaji wa maji katika Mji wa Tarime.
Kwa upande wake, akiwasilisha mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2026 Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya mipango na Uratibu Bwana Emmanuel Mazengo amesema kwa mwaka 2025/2026 Mkoa wa Mara unatarajia kukusanya mapato ya ndani yanayokadiria kufikia 47,194,453,000.
“Mapato hayo yameongezeka ukilinganisha na mapato yaliyoidhinishwa mwaka wa fedha 2024/2025 shilingi 36,998,164,000 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 27.6” amesema Bwana Mazengo.
Bwana Mazengo amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Mkoa wa Mara unatarajia kutumia jumla ya shilingi 380,578,762,000 kwa ajili ya mishahara, matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo.
“Hili ni ongezeko la asilimia 2.3 ukilinganisha na kiasi cha shilingi 372,140,130,000 kilichoidhinishwa mwaka 2024/2025 na ongezeko linatokana na kuongezeka kwa fedha za maendeleo na matumizi mengine yanayotokana na mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa” amesema Bwana Mazengo.
Bwana Mazengo amesema vipaumbele vya bajeti ya Mkoa wa Mara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ni kuendelea na uboreshaji wa sekta ya elimu, huduma za afya, huduma za utawala na kuweka mazingira wezeshi na kuboresha usimamizi wa uchumi na uzalishaji.
Bwana Mazengo amesema miradi ya maendeleo inayotegemewa kutekelezwa ni pamoja na ukamilishaji wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, ujenzi wa nyumba ya kupumzikia viongozi, ununuzi wa gari, ukarabati wa nyumba ya Mkuu wa Mkoa na usimamizi wa mitihani.
Kikao cha RCC leo pamoja nan ambo mengine kimepitia taarifa za miradi ya sekta ya Maji ambapo taarifa zinaonyesha kuwa Mji wa Tarime wananchi wanaopata maji safi na salama ni asilimia 52.6 tu huku kukiwa na mradi mkubwa utakaofikisha maji katika Mji huo kutoka Ziwa Victoria ambao haujakamilika.
Aidha, kikao hicho pia kimepitisha Jimbo la Uchaguzi la Serengeti kugawanywa na kupata majimbo mawili ya uchaguzi na majina ya majimbo yanayopendekezwa ni Serengeti Mashariki na Serengeti Magharibi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa