Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mara (RCC) na kuzipongeza Halmashauri ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani ambapo hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2024 Halmashauri hizo zimekusanya shilingi bilioni 16.516 sawa na asilimia 107 ya lengo la makusanyo kwa muda huo.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji, Mhe. Mtambi amesema makusanyo hayo ni sawa na asilimia 45 ya makusanyo yaliyopangwa kukusanywa katika mwaka wa fedha 2024/2025.
“Ninazipongeza zaidi Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambazo zimekusanya kwa zaidi ya asilimia 50 ya makusanyo yaliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameitaka Halmashauri ya Mji wa Tarime kuweka mikakati vizuri ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha inafikia asilimia 100 ya makusanyo hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kuvipongeza vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi katika Mkoa wa Mara kwa ushirikiano walioutoa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Mkoa wa Mara.
Aidha, amewataka viongozi kuwahamasisha wananchi kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kulima mazao ya chakula na biashara ili kuimarisha uchumi wa familia zao, Mkoa na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Menejimenti ya Ufuatiliaji na Ukaguzi (MMI) Bwana Marco Maduhu amesema kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambayo katika mpango wa makusanyo hadi mwisho wa Novemba ilitakiwa kukusanya 4,754,526,589 lakini imefanikiwa kukusanya milioni 6,662,423,141.
“Mwenendo wa makusanyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ni mzuri na hali hii ikiendelea kuna uwezekano wa Halmashauri kukusanya asilimia 100 au zaidi ya bajeti yake yam waka 2024/2025” amesema Bwana Maduhu.
Bwana Maduhu amesema Halmashauri ya Mji wa Tarime imefanikiwa kukusanya asilimia 26 tu ya mpango wake wa makusanyo ya mwaka na kuonya kwamba hali ikiendelea hivi kuna uwezekano Halmashauri kushindwa kufikia lengo la kukusanya mapato kwa asilimia 100 ya bajeti ya mwaka 2024/2025.
Bwana Maduhu amezitaka Halmashauri kuongeza juhudi za kukusanya mapato ya ndani na kuhakikisha wanadhibiti mianya ya upotevu wa mapato, matumizi sahihi ya mfumo wa kukusanyia mapato wa kielekroniki (TAUSI) na kuhakikisha kamati za mapato zinafanyakazi kwa ufanisi na kuzingatia mwongozo wa usimamizi wa mapato ya Halmashauri wa mwaka 2019.
Aidha, Bwana Maduhu amezitaka Halmashauri kuendelea kufanya tathmini ya uwezo wa vyanzo vya mapato vilivyopo na kubuni vyanzo vipya ya mapato na kuzitaka Halmashauri zenye sababu ya msingi zitakazosababisha kushindwa kukusanya kwa mujibu wa malengo kuomba kupunguzia bajeti kabla ya Februari, 2025.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa, wabunge, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya na viongozi wa taasisi za umma.
Wengine walioshiriki kikao hicho ni Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Mipango wa Halmashauri, baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa