Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 na kuwapongeza wadau wote wa uchaguzi wakiwemo viongozi na watendaji wa Serikali wa Mkoa wa Mara kwa usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa shughuli za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema viongozi na watendaji wa Serikali wa Mkoa wa Mara wametoa ushirikiano mkubwa uliofanikisha kila hatua ya zoezi la uchaguzi na kuwataka viongozi hao kuendelea kutoa ushirikiano katika mazoezi mengine ya kimkoa na kitaifa yatakayofanyika hapo baadaye.
“Mkoa wa Mara umekuwa na kelele kidogo katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwa kila mmoja ametimiza wajibu wake na ametoa ushirikiano kwa wengine katika kusimamia na kufanya mambo mbalimbali kufanikisha uchaguzi huu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa miongozo, fedha na vifaa vya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa wakati jambo ambalo limeongeza uhamasishaji wa wananchi kushiriki kujiandikisha, kugombea na kupiga kura katika uchaguzi huu.
Aidha, Mhe. Mtambi amevipongeza vyama vya siasa, taasisi za dini, viongozi wa kimila, mashirika binafsi na wadau wote wa uchaguzi katika Mkoa wa Mara kwa namna walishohamasisha wananchi kushiriki zoezi la uchaguzi kwa amani na utulivu wakati wote wa uchaguzi.
Kanali Mtambi amevipongeza vyombo vya dola vikiongozwa na Jeshi la Polisi kwa namna ambavyo vimeshiriki kikamilifu katika kusimamia na kuratibu zoezi zima la uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akitoa taarifa ya Mkoa wa Mara, Afisa Serikali za Mitaa Bi. Agness Kimei amesema Mkoa uliandikisha jumla ya wapiga kura 965,860, baada ya pingamizi wapiga kura 965,859 wakati siku ya uchaguzi wapiga kura 773,213 walijitokeza ambao ni sawa na asilimia 80.1.
“Katika nafasi za Wenyeviti wa vijiji zilizogombaniwa zilikuwa 458 kati ya hizo Chama cha Mapinduzi kimeshinda nafasi 446 sawa na asilimia 97, CHADEMA kimeshinda nafasi 12 ambazo ni sawa na asilimia tatu” amesema Bi. Kimei.
Bi. Kimei amesema Mwenyekiti wa Mitaa zilikuwa 238 na kati ya hizo CCM kimeshinda nafasi 232 sawa na asilimia 97 wakati CHADEMA wameshinda nafasi sita ambazo ni sawa na asilimia tatu na kwa nafasi za Mwenyekiti wa Kitongoji zilizogombaniwa 2,502 kati ya hizo CCM walishinda nafasi 2,403 sawa na asilimia 96 na CHADEMA walishinda nafasi 98 sawa na asilimia nne huku kitongoji kimoja uchaguzi utarudiwa tena.
Bi. Kimei amesema kuwa baadhi ya changamoto zilizokuwepo wakati wa zoezi la uandikishaji wananchi walichanganya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura lililokuwa limefanyika kabla ya zoezi la uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Bi Kimei ameshauri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi na waratibu wa Mkoa kuhusu uandaaji wa taarifa mbalimbali pamoja na kuandaa fomati mapema ili zijadiliwe na waandaaji wa taarifa ili kuepuka ucheleweshaji wa taarifa.
Aidha, ameshauri kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa ziboreshwe kwa kuhakikisha kuwa fomu zote muhimu zinakuwepo kwenye kanuni ili kuepuka changamoto wakati wa kuanza kuzitumia na kuzalisha fomu husika.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime Bwana Saul Mwaisenya amesema katika uchaguzi uliofanyika tarehe 27 Novemba, 2024, kitongoji cha Komerera, katika Kijiji cha Komorera, Wilaya ya Tarime wagombea wa CCM na CHADEMA walipata kura sawa.
Bwana Mwaisenya amesema kutokana na wagombea hao kupata kura sawa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika kitongoji hicho unatarajiwa kurudiwa baada ya siku 14.
Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, baadhi ya maafisa wa Sekretarieti ya Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri na waratibu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutoka Halmashauri zoteza Mkoa wa Mara.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 umefanyika tarehe 27 Novemba, 2024 hapa nchini ukiwa na kauli mbiu “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa