Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amepiga kura kuwachagua viongozi wa Serikali ya Mtaa katika kituo kilichopo Ofisi ya Kata Mukendo, Manispaa ya Musoma na kuwapongeza wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ukomavu wa kisiasa na kuwataka wajitokeze kwa wingi kupiga kura.
Akizungumza mara baada ya kupiga kura Mhe. Mtambi amesema katika kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa wananchi wameonyesha ukomavu wa kisiasa uliosababisha kampeni kufanyika kwa amani na utulivu na hamna malalamiko ya vyama au wagombea kufanyiwa fujo wakati wa kampeni.
“Ninawapongeza wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ukomavu mkubwa wa kisiasa waliouonyesha katika kipindi chote cha kampeni na ninawakumbusha kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amevitaka vyama vya siasa na wanachama wao kuheshimu na kuzifuata kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambazo walishiriki kuzitunga na kama kuna malalamiko yoyote wanaweza kuwasilisha malalamiko hayo sehemu zinazohusika kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amepiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima wakati huu wa uchaguzi na kuwataka wananchi kuhakikisha kuwa baada ya kupiga kura wanaenda kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Mhe. Mtambi amewaonya watu wanaopanga kufanya vurugu na kuahidi kuwa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara na wananchi wa Mkoa wa Mara hawatamvumilia mtu yoyote atakayeanzisha fujo katika kipindi hiki na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itawachukulia hatua za kisheria watu wote wanaoanzisha vurugu wakati huu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka akizungumza katika eneo hilo amewaomba wananchi wa Wilaya ya Musoma kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi na kuwahakikishia usalama wao wakati wote wa uchaguzi.
Mhe. Chikoka pia amewataka wananchi kuachana na mikusanyiko isiyo ya lazima na kutoa taarifa kwa viongozi wanapohisi kuna uwezekano wa uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa mbili kamili asubuhi na vinategemewa kufungwa saa 10 jioni na baada ya kupiga kura wananchi wanashauriwa kuondoka katika eneo la kituo cha kupiga kura kwa utulivu na amani.
Leo ni siku ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo wananchi wanachagua viongozi mbalimbali wakiwemo wenyeviti wa Mitaa/Vijiji, wajumbe wa serikali ya mtaa/kijijji, wenyeviti wa vitongoji na kauli mbiu ya mwaka huu ni Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa