Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, Mkuu wa Mkoa wa Mara leo tarehe 26 Machi, 2025 ameendelea na ziara yake katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali katika Manispaa ya Musoma na ametoa saa 48 taasisi za umma zilizoathirika na tukio hilo ziwe zimekarabati maeneo yao na kurejesha huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika ziara ya Kamati ya Usalama ya Mkoa leo tarehe 26 Machi, 2025 Mhe. Mtambi amezitaka taasisi za umma kuonyesha mfano kwa wananchi kwa kuurejesha Mji wa Musoma katika mazingira yake ya awali.
“Ninatoa saa 48 taasisi zote za umma ziwe zimekarabatiwa na kurejesha huduma zake kama ilivyokuwa awali kabla ya maafa hayo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ametoa saa 12 kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kukarabati vituo vya polisi vilivyoharibiwa katika tukio hilo ili vituo hivyo viendelee kufanyakazi na kuimarisha ulinzi wa wananchi katika maeneo yaliyoathirika.
Mhe. Mtambi ametoa siku 7 kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kurejesha taa za barabarani zilizoathiriwa na maafa hayo katika Manispaa ya Musoma.
Mhe. Mtambi ametoa saa 8 kwa TEMESA na TANESCO kuweka umeme katika majengo ya NFRA yanayotumika kama kituo cha kuwahifadhi waathirika wa maafa hayo kilichopo katika eneo la Baruti Manispaa ya Musoma.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi amelipongeza Shirika la Umeme TANESCO Mkoa wa Mara kwa kuweza kurejesha umeme katika maeneo yote ya Manispaa ya Musoma na kutoa agizo kuwa hadi saa sita mchana leo TANESCO iwe imeondoa mabaki ya nyaya na nguzo zilizoharibika katika maeneo yote ya wananchi ili kupunguza taharuki kwa wananchi wa Musoma.
Mhe. Mtambi ameliagiza Jeshi la Magereza Mkoa wa Mara kuondoa miti yote iliyoanguka katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Musoma na hususan maeneo ya shule ili watoto waweze kupita kwa urahisi na kurejesha hali ya awali katika maeneo hayo.
Mhe. Mtambi amewapongeza Walimu Wakuu wa shule za Msingi Iringo A na B kwa kuwaunganisha wanafunzi wa baadhi ya madarasa wasome pamoja baada ya madarasa kadhaa ya shule hizo kuezuliwa na upepo.
Mhe. Mtambi amesema kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha, Kamati ya Maafa ya Mkoa na Wilaya zijipange kwa ajili ya kuwapokea waathirika wengi zaidi na kuhakikisha huduma zote muhimu kwa waathirika hao zinapatikana.
Akizungumza katika ziara hiyo, Meneja wa TARURA Mkoa wa Mara Mhandisi William Lameck amesema barabara na hususan mitaro na taa katika maeneo mengi zimeathiriwa na maafa hayo na tayari wamefanya tathmini na wamepata baadhi ya wazabuni wa kurejesha huduma hizo kwa haraka.
“Mitaro inaanza kusafishwa kuanzia leo wakati taa tayari mzabuni amepatikana kwa ajili ya kununua taa mpya zitakazowekwa katika maeneo yaliyoathiriwa na upepo huo” amesema Mhandisi Lameck.
Mhe. Juma Chikoka, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, akizungumza katika ziara hiyo, amesema awali waathirika waliojitokeza kuhitaji msaada walikuwa watu 29 kutoka kaya tisa hata hivyo, wananchi wameendelea kuongezeka na kutambuliwa na viongozi wao wa Mitaa na Kata.
Mhe. Chikoka amewataka wananchi ambao wameathirika na hawana sehemu ya kulala kwa sasa wafike katika kituo hicho ili kupata msaada ikiwemo sehemu salama ya kulala, chakula na huduma nyingine za kibinadamu.
Katika ziara hiyo Mhe. Mtambi pia amewapokea maafisa wawili ambao ni Waratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa, Bwana Salvatory Katamaza na Sactarius Liliwa ambao wameungana na timu za uratibu wa Maaafa Mkoa na Wilaya kushughulikia tatizo hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa