Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 5 Machi, 2025 ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji na kuwataka Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara kufanya msako wa kuwatafuta na kuwachukulia hatua wafafunzi wa kidato cha kwanza ambao hawajaripoti shule.
“Wakuu wa Wilaya anzeni msako katika maeneo yenu kuwatafuta hawa wanafunzi ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na mpaka sasa hawajasajiriwa na kuhakikisha wote wanasajiriwa na kuanza masomo mapema iwezekanavyo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuwa ni asilimia 82.3 tu ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ndio wamejisajiri mpaka tarehe 04 Machi, 2025 jambo ambalo amesema halikubaliki.
Mhe. Mtambi amesema hadi tarehe 04 Machi, 2025 wanafunzi wa awali waliosajiriwa walikuwa ni asilimia 99.61 huku waliosajiliwa darasa la kwanza walikuwa wamefikia asilimia 107 huku wanafunzi wa kuanza kidato cha kwanza wakiwa asilimia 82.3 tu ya wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya kuwakamata wazazi wote ambao watoto wao hawajaripoti shuleni na kuwachukulia hatua za kisheria na kuongeza kuwa kuna taarifa watoto hawa hawajaripoti shuleni kwa sababu wanajihusisha na uchimbaji wa madini, kuolewa na wengine ni uzembe tu wa wazazi.
Mhe. Mtambi amesema Serikali imewekeza fedha nyingi sana kujenga shule na kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia lakini haitakuwa na faida inayotarajiwa kama watoto hawatapelekwa shule kujifunza.
“Mkoa wa Mara hautamfumbia macho mzazi yoyote atakayemkosesha mtoto kupata haki yake ya masomo” amesema Mhe. Mtambi na kukihakikishia kikao hicho kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wazazi wote wanaozembea kuwapeleka watoto shule.
Mhe. Mtambi pia amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kuwasilisha mpango na bajeti ya ukarabati wa shule chakavu zilizopo kwenye maeneo yao mwishoni mwa Aprili, 2025 na kuwataka wabunge kuwasilisha orodha ya shule chakavu zilizopo kwenye majimbo yao ili aweze kuziangalia orodha zote mbili na kujiridhisha.
Aidha, amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula mashuleni ili waweze kujifunza vizuri na kuboresha ufaulu.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara Mhe. Ghati Zephania Chomete amesema suala la chakula mashuleni kutokana na umuhimu wake, Mkoa uwekeze kwenye kutoa elimu kwa wananchi ili wapate uelewa kuhusu umuhimu wa wao kuchangia.
“Tunatakiwa kuwaelimisha kuhusu tafiti za kitaalamu zilizofanyika kuhusu wanafunzi wanaokula shuleni wanavyofaulu ukilinganisha na wanafunzi ambao hawali chakula shuleni” amesema Mhe. Chomete.
Aidha, Mhe. Chomete amewataka wasimamizi wa Elimu kuhakikisha kuwa shule ambazo zina maeneo makubwa au mashamba zipewe maelekezo ili mashamba hayo yaweze kulimwa kwa ajili ya chakula cha wanafunzi.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Maridhiano na Amani ya Mkoa wa Mara Shehe Juma Masiroli amesema yeye ni mhamasishaji wa chakula mashuleni katika Mkoa wa Mara, ametembelea shule nyingi katika Manispaa ya Musoma sio shule nyingi zinatoa chakula shuleni kwa wanafunzi wote.
“Ni shule tatu tu za Serikali katika Manispaa ya Musoma ndio zinazotoa chakula kwa wanafunzi wote kwa asilimia 100 huku shule nyingi zinatoa kwa wanafunzi wachache wanaochangia” amesema shehe Masiroli.
Shehe Masiroli ametoa sababu mbalimbali zinazochangia ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanafunzi kuwapotosha wazazi kuwa chakula kinaliwa na walimu, umaskini miungoni mwa wazazi na walezi, siasa katika baadhi ya maeneo zinaathiri michango.
Bwana Masiroli ameishauri Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wahamasike kutoa chakula mashuleni na wanafunzi waweze kusoma vizuri na wanafunzi wengine hata majumbani wakirudi hawana uhakika wa kupata chakula na hivyo kuwalazimisha kulala njaa wakiwa wameshinda na njaa.
Jumla ya wanafunzi 46,671 ambao ni sawa na asilimia 17.7 ya wanafunzi waliopangiwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Mkoa wa Mara hawajaripoti shule kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uzembe wa wazazi, uchimbaji wa madini na ajira za watoto.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa