Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 28 Machi, 2025 ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi katika Shule ya Sekondari ya Butuguri na kuutaka uongozi wa Wilaya kuhakikisha kuwa wanafunzi wa shule hiyo wanapata walau mlo mmoja wakiwa shuleni.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Nne wa shule hiyo na kumtaka Mkuu wa Wilaya kama wazazi watagoma kuchangia chakula kwa hiari wachukuliwe hatua za kisheria kuwawezesha wanafunzi waweze kusoma vizuri.
“Hili sio la kubembeleza, haya ni maamuzi ya Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi waweze kusoma vizuri, kama hawataki kuchangia kwa hiari wachukuliwe hatua” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe. Moses Kaegele kukutana na wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Butuguri ili kuweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo wanapata angalau mlo mmoja shuleni.
Aidha, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuangalia uwezekano wa kuajiri walimu wa muda katika shule hiyo ili kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo ya Sanaa na lugha katika shule hiyo.
Akikagua mradi wa ujenzi wa mabweni na madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano katika shule hiyo, Mhe. Mtambi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kwa kuwabadilisha wakandarasi waliopewa zabuni ya kujenga mabweni na madarasa ya kidato cha tano na sita katika shule hiyo.
“Ninawapongeza kwa kuwabadilisha wakandarasi waliopewa kazi ya kujenga mabweni na madarasa katika mradi huu na kuufanya mradi uendelee baada ya changamoto zilizokuwa zimejitokeza” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Mara kuacha kuutaja Mfumo wa Manunuzi ya Serikali (NEST) kama sababu ya kuchelewa kwa miradi na badala yake amezitaka kutoa mafunzo zaidi kuhusiana na matumizi ya mfumo huo kwa watendaji na wazabuni mbalimbali wanaohusika katika utekelezaji wa miradi ili wautumie mfumo vizuri.
“Changamoto kubwa ni watumiaji wa mfumo huu, Halmashauri toeni mafunzo kwa wazabuni ambao wanauwezo wa ktekeleza miradi na hawajaujua mfumo na maafisa wanaosimamia utekelezaji wa miradi ili kukabiliana na changamoto hiyo” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Butuguri Mwalimu Nyamtelele Christopher amesema Shule hiyo ilipokea shilingi 510,448,303.78 kutoka Serikali Kuu, SEQUIP, na EP4R kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa mabweni, madarasa na matundu ya vyoo kwa nyakati tofauti kuanzia tarehe 11 Juni, 2024.
Mwalimu Christopher amesema ujenzi wa madarasa na bweni moja na madarasa manne umekamilika huku ujenzi wa madarasa manne upo kwenye ukamilishaji, ujenzi wa bweni moja upo hatua ya kupandisha kuta wakati bweni linguine lipo hatua ya msingi na ujenzi wa matundu ya vyoo upo kwenye ukamilishaji.
Mwalimu Christopher amesema changamoto kubwa katika utekelezaji wa mradi huo ni matumizi ya mfumo wa NEST, kukosekana kwa maji eneo la mradi na mvua kubwa iliyoathiri upelekaji wa vifaa eneo la mradi.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama, baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi na maafisa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa