Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kukumbushia agizo lake la kushikiria posho za viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mpaka madawati yaliyotengewa fedha yawe yamewafikia wanafunzi.
Mhe. Mtambi alitoa agizo hilo tarehe 26 Februari, 2025 akiwa katika ziara ya kawaida Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na leo kulirudia tena katika kikao cha RCC wakati wa majadiliano ya mipango na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026
“Kama madawati hayo hayatapelekwa shuleni kwa wakati hata mimi posho yangu nikija Tarime msinipe mpaka wanafunzi watakapopata madawati” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameutaka Mgodi wa North Mara kumpatia taarifa za maendeleo ya utengenezaji wa madawati hayo ili aweze kujua nani anayekwamisha utengenezaji wa madawati hayo na kuwafanya wanafunzi kukosa madawati huku fedha zikiwa zimetengwa kwa muda mrefu bila kununua madawati hayo.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kufuatilia zabuni zinazotangazwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ili waweze kunufaika na utekelezaji wa miradi ya CSR katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Mhe. Mtambi amewataka wazabuni watakaopata zabuni za kutekeleza miradi hiyo kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na huduma zitakazotolewa na miradi hiyo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara Bwana Hermence Christopher amesema utekelezaji wa miradi ya CSR katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imechelewa kutokana na taratibu mpya za manunuzi ndani ya mgodi.
Bwana Christopher amesema taratibu zinautaka mgodi kwenye manunuzi yote makubwa kupata kibali Tume ya Madini na manunuzi ya miradi ya CSR yalikuwa ni ya shilingi zaidi ya bilioni tisa hivyo taratibu za kisheria ilibidi zifuatwe na hivyo kuchelewesha manunuzi.
“Kwa sasa kibali kimepatikana na matangazo zabuni yameshasambazwa ili kuwapata wazabuni watakaotekeleza miradi hiyo ikiwemo utengenezaji wa madawati kwa ajili ya wanafunzi wa Shule za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime” amesema Bwana Christopher.
Bwana Christopher amesema wanategemea kutoa kazi ya kutengeneza madawati kwa wazabuni wengi na wanategemea kuanza kutengeneza madawati wiki ijayo na yatakuwa yakisambazwa kwa kadiri yanavyokamilika.
Bwana Christopher amekihakikishia kikao hicho kuwa Mgodi huo unategemea mpaka tarehe 31 Machi, 2025 madawati yatakuwa yametengenezwa na kusambazwa katika shule zenye upungufu wa madawati katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa