Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo amefungua kongamano la Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Mara na kuwataka viongozi wa vyama vya ushirika kuongeza ubunifu katika kutumia fursa zilizopo ili kujenga uchumi wa wanaushirika.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi iliyofanyika katika ukumbi wa Mwembeni Complex, Manispaa ya Musoma Mhe. Mtambi amesema ushirika ukitumiwa vizuri unaweza kumaliza tatizo la upatikanaji wa mtaji wa biashara katika sekta mbalimbali.
“Kwa sasa Serikali ya Mkoa wa Mara inasimamia uendeshaji wa vyama vya ushirika kwa karibu sana na niwatahadharishe tu viongozi kutojihusisha na ubadhilifu wa mali za ushirika, huo utakuwa ni sawa na uhujumu uchumi, hatutakubali hilo litokee na likitokea hatua kali za kisheria zitachukuliwa”amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kwa kushirikiana na wataalamu wa kilimo kuchukua hatua za kudhibiti utoroshaji wa mazao ya kimkakati ikiwa ni pamoja na kusimamia uuzaji wa mazao kupitia mfumo wa skatabadhi ghalani ili uweze kutumika katika ununuzi wa mazao mengi ya wananchi.
Mhe. Mtambi amesema suala la vyama kujiunga kwenye mfumo wa MUVU sio la hiari na kutoa hadi tarehe 30 Juni, 2025 vyama vyote vya ushirika Mkoa wa Mara viwe vimejiunga na mfumo wa MUVU na kuwataka Wakuu wa Wilaya kufuatilia utekelezaji wa suala hilo.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wanaushirika wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ili kuwachagua viongozi watakaoliletea maendeleo Taifa la Tanzania.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Mara Bwana Samwel Gisiboye akisoma risala ya jukwaa hilo amesema Mkoa wa Mara una jumla ya wanachama 21,963 na wasio wanachama 11,665 wanaohudumiwa na vyama vya ushirika.
Bwana Gisiboye amesema Mkoa wa Mara una jumla ya vyama vya ushirika 308 lakini kati ya hivyo vyama vya ushirika 283 tu ndio vimesajiriwa katika mfumo wa MUVU na maafisa ushirika 11 huku kukiwa na upungufu wa maafisa ushirika 12 ii kuhudumia wanaushirika wa Mkoa wa Mara.
“Vyama vya akiba na Mikopo (SACCOS) katika Mkoa wa Mara vina mtaji wenye thamani ya shilingi 5, 280,008,536 na vimewezesha mikopo ya shilingi 6,395,015,531 kwa wananchama wake” amesema Bwana Gisiboye.
Bwana Gisiboye amesema vyama vya ushirika vimewekeza katika miradi mbalimbali yenye thamani ya shilingi 28,281,953,062.67 na kuwezesha utoaji wa ajira za 490 za kudumu na za muda na jumla ya shilingi 29,000,000 kimewekezwa katika Hisa za Benki ya Ushirika Tanzania (COOP Bank).
Bwana Gisiboye ameelezea manufaa waliyopata wakulima wa Choroko katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Halmashauri ya Mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambao waliuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na bei ya zao hilo imeongezeka karibia mara mbili kwa kilo moja.
Amesema dira ya Jukwaa la Ushirika katika Mkoa wa Mara ni kuwa na baraza huru, imara na endelevu la wanaushirika lenye taswira ya kuche hemusha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ufunguzi wa kongamano hilo limehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika, wawakilishi kutoka Benki ya Ushirika Tanzania, wadau wa ushirika na viongozi wa vyama vya ushirika.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa