Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima tarehe 09 Desemba, 2024 amekuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na kuupongeza mkoa wa Mara kwa kufanikiwa kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza katika maadhimisho hayo ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe, Wilaya ya Tarime, Mhe. Gwajima amesema Mkoa wa Mara siyo kinara tena wa vitendo vya ukatili wa kijinsia hapa nchini.
“Tuiambie dunia ijue kuwa Mara imefanikiwa kushusha takwimu za ukatili wa kijinsia; na kama inawezekana Mara na Mikoa mingine inawezekana” amesema Dkt. Gwajima.
Mhe. Gwajima amesema kati ya Mikoa inayoongoza kwa matukio ya ukatili nchini ni Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara ambayo ina asilimia 43 kila mmoja huku Mkoa wa Mara ukishika nafasi ya tatu ukiwa na asilimia 28.
Mheshimiwa Gwajima ameitaja mikoa mingine yenye ukatili wa kijinsia ni Mkoa wa Singida asilimia 20, Mkoa wa Tanga asilimia 19 na Mkoa wa Dodoma asilimia 18.
Dkt. Gwagima ameutaka Mkoa wa Mara kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia kwa kupeleka elimu zaidi kwa makundi mbalimbali ya wananchi ili kuwajengea uelewa kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia.
Mhe. Gwajima amewapongeza wadaua wote likiwemo Jeshi la Polisi Tanzania, taasisi za umma na binafsi ambazo zimeungana kwa pamoja kusaidia kupunguza matukio kwa kutoa elimu na kuchukua hatua za kisheria pale inapohitajika.
Akizungumza wakati akimkaribisha Mhe. Gwajima, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya amesema Desemba 09 ya kila mwaka ni siku ya uhuru wa Tanzania Bara na sikukuu hii kwa Mkoa wa Mara inatumika kupinga ukatili wa kijinsia.
Bwana Kusaya amesema haya ni mapambano ya watu wote wananchi na viongozi na kwa Mkoa wa Mara shabaha yetu ni moja kumlinda mtoto na watu wenye mahitaji maalum.
“Kumlinda mtoto ni kumuunga mkono Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amenuia kumlinda mtoto wa Tanzania kwa gharama yoyote ile” amesema Bwana Kusaya.
Akizungumza katika hitimisho hilo la siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara Bwana Apolinary Lyambiko amesema kuwa mgodi huo unasaidia juhudi za kupinga ukatili wa kinjisia hapa nchini.
“Tumepokea tuzo saba katika kusimamia dhamira ya uwajibikaji katika jamii ikiwamo Kupinga Ukatili wa Kijinsia nchini Tanzania” amesema Bwana Lyambiko.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/ Rorya, Mark Nyera amemthibitishia Waziri Gwajima kuwa kampeni ya Kupinga ukatili wa Kinjisia, siku hizi 16 zimetumika vizuri kupaza sauti juu ya suala hilo.
Afande Nyera amesema makosa ya ukatili wa kinjisia kwa sasa yanapungua kutoka mwaka mmoja kwenda mwingine mathalani kutoka mwaka 2023 kwenda 2024 yakiwa chini ya matukio 2000.
Kamanda Nyera akisema kuwa siku hizo 16 zinahitimishwa siyo kwamba Jeshi la Polisi Tanzania linaweka silaha chini bali linaongeza nguvu katika mapambano hayo kwa kasi zaidi.
Wakati huo huo, Mhe. Dkt. Gwajima amekabidhi majiko ya gesi 222 kwa wananchi wa vijiji vinavyouzunguka mgodi wa Barrick North Mara yaliyotolewa na mgodi huo kwa lengo la kuwaepushia wananchi adha ya matumizi ya nishati ya kupikia isiyo salama.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Serikali na taasisi za binafsi, watendaji wa Serikali na wananchi wa Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa